Serikali, viongozi wa dini wajadili kutokomeza uhalifu

Dodoma. Katika kukabiliana na matukio ya uhalifu yanayotokea katika jamii Serikali imefanya kikao maalumu na viongozi wa dini chenye  lengo la kudhibiti matukio ya uhalifu.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika jijini Dodoma leo Mei 17, 2024 Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amewaomba viongozi hao wa dini kuendelea kuisaidia na isichoke kuishauri Serikali katika kudumisha amani na usalama.

“Wajibu wa Jeshi la Polisi ni kuhakikisha ulinzi wa raia na mali zao unaimarika na amani inatawala nchini ili kuwezesha wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi na kijamii.”

“Kwenye kutekeleza wajibu huo Jeshi la Polisi ushirikiano na jamii na wadau wengine katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 makosa makubwa ya jinai yaliyoripotiwa katika vituo vya Polisi yamepungua kutoka 45,485 hadi 43,146 sawa na asilimia tano ikilinganishwa na kipindi cha mwaka 2022/23.

“Hivyo nawaomba viongozi wa dini kuunga mkono Serikali katika maeneo mnayotoka kwa kukemea ili kudhibiti uhalifu.”

Akizungumza kwenye kikao hicho, Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakari Zubeir amesema ni uamuzi mzuri kwa Serikali  kuhusisha viongozi wa dini katika mapambano dhidi ya uhalifu, huku wakiitaka kutochoka kuwaita yanapotokea matatizo mbalimbali ili kuendelea kuimarisha uhusiano huo.

Akizungumzia usajili wa taasisi za kidini, Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki Mbeya na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Gervas Nyaisonga amesema Serikali ipitie upya katiba za vikundi mbalimbali vya kidini.

“Kupitia katiba zetu ndio Serikali itajua msingi wa shughuli za taasisi hizo za kidini ili kuepusha baadhi ya uhalifu ambao pia unatokea katika baadhi ya taasisi au vikundi vya kidini,” amesema Nyaisonga.

Naye, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Alex Malasusa amesema Serikali kwa sasa wamepata mahali pa kuzungumza na kuweka mikakati ya pamoja na viongozi wa dini.

“Kwa sasa sisi viongozi wa dini na Serikali  tunaweza kuzungumza na kuweka mikakati ya pamoja katika mapambano dhidi ya uhalifu na kukubaliana juu ya maazimio yaliyofikiwa, ili kudumisha amani na usalama nchini,” amesema Dk Malasusa.

Related Posts