Dar es Salaam. Katika kuonyesha uhusiano wa karibu baina ya Tanzania na China, Serikali ya nchi hiyo imetoa mchango wa Sh 1.3 bilioni kwa ajili ya kusaidia waathirika wa mafuriko ya mvua yaliyoikumba Tanzania mwaka huu.
Maeneo kadhaa ya Tanzania yameathiriwa na mvua kubwa za masika zilizochanganyika na zile za El Nino na Waziri wa Mambo ya Nje nchini China, Wang Yi amesema Wachina wamesikia kuhusu athari hizo na wametoa mchango huo ili kusaidia waathirika kuanza upya maisha yao.
Katika mkutano wa pamoja uliofanyika jijini Beijing, China, leo Mei 17,2024 Wang Yi amesema katika miaka 60 iliyopita nchi hizo mbili zimejipambanua kuwa rafiki wa kwenye shida na raha.
“Tanzania mara zote amekuwa rafiki wa China, miaka 60 ina maana kubwa sana kwenye uhusiano hivyo hatua inayofuata baada ya hapa ni kuendeleza uhusiano huu katika zama mpya za kujenga dunia yenye maendeleo, ya haki na usalama kwa watu wote,” amesema Wang.
Katika hatua nyingine, Serikali ya China leo imetoa mwaliko rasmi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhudhuria mkutano wa masuala ya usalama baina ya China na Afrika (FOCAC) uliopangwa kufanyika Septemba mwaka huu.
Mkutano huo wa FOCAC hufanyika kila baada ya miaka mitatu na katika miaka ya karibuni umekuwa ni miongoni mwa mikutano muhimu kwenye uhusiano wa kimkakati baina ya nchi za Afrika na China.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema Tanzania inathamini mchango wa taifa hilo la bara la Asia katika maendeleo yake, hivyo wakati umefika wa kuingia katika zama mpya kuendana na changamoto za dunia ya sasa.
“China ni rafiki zetu kwenye nyakati zote, ambaye anatabirika na habadilikibadiliki wakati wote. Baada ya miaka hii 60 ya uhusiano uliotukuka, sasa tuingie katika zama mpya za uhusiano ambao utazingatia changamoto zilizopo kwenye kujenga dunia bora zaidi kuliko ile iliyokuwepo wakati wa waasisi wa uhusiano huu,”amesema Makamba.
Pia, Makamba ameshukuru kwa mchango uliotolewa na China wa kusaidia wananchi walioathirika na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kwa nyakati tofauti, akisema kuwa huo ni ushahidi mwingine wa urafiki wa kipekee baina ya nchi hizo mbili.
Katika ziara yake hiyo inayoendelea nchini China, Makamba alitembelea na kufanya mazungumzo na taasisi, viongozi wa mashirika yanayohusika na misaada kwa Tanzania ikiwemo benki ya EXIM ambayo imeahidi kuendelea kukopesha kwenye miradi ya kimkakati
Katika kuendeleza uhusiano, China imekubali ombi la Tanzania la kufanya maboresho ya Chuo cha Diplomasia cha Dk Salim Ahmed Salim ikiwemo kuongeza majengo, mitaala na kukifanya cha kutengeneza ajenda kwa ajili ya masuala ya kimkakati ya kubadili mfumo wa uendeshaji wa dunia.
Dk Salim ni mmoja wa wana diplomasia wa Tanzania wenye heshima kubwa nchini China na uamuzi wa kuongeza hadhi ya chuo hicho umezingatia hadhi yake kidiplomasia na umuhimu wake kwa nchi hizo mbili.