Shule za kidato cha tano zaongezeka kwa asilimia 48

Dodoma. Idadi ya shule za kidato cha tano na sita imeongezeka kutoka 318 mwaka 2016 hadi kufikia 615 mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 48.2.

Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Zainab Katimba ameyasema hayo leo Mei 17,2024 wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki.

Mbunge huyo amehoji Serikali ina mkakati gani wa kuongeza shule za sekondari za kidato cha tano na sita kwa kuzingatia umoja na kulinda utaifa.

Akijibu swali hilo, Zainab amesema Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kujenga na kupanua shule za sekondari za kidato cha tano na sita za kitaifa.

Amesema lengo ni kukidhi uwepo wa ongezeko la wanafunzi wa kidato cha tano na sita nchini kufuatia mafanikio ya utekelezaji wa Sera ya Elimu bila ada iliyoanza kutekelezwa mwaka 2016.

Amesema idadi ya shule za kidato cha tano na sita imeongezeka kutoka 318 mwaka 2016 hadi 615 mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 48.2

Amesema katika mwaka wa fedha wa 2024/2025, Serikali kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP), imepanga kujenga shule za bweni za wavulana za kitaifa saba zitakazochukua  wanafunzi 1,080 kwa kila moja.

Aidha, Zainab amesema Serikali inaendelea na mpango wa ukamilishaji wa ujenzi wa shule za sayansi za bweni za wasichana 26.

“Serikali itaendelea na jitihada zake za kuongeza ujenzi na upanuzi wa shule za kitaifa za bweni za kidato cha tano na sita lengo likiwa ni  kuhakikisha wanafunzi wote wanapewa fursa ya kusoma,”amesema.

Katika swali la nyongeza, Ndaki amesema katika sera ya elimu inataka watoto wasome kuanzia awali hadi kidato cha nne katika kata husika alikozaliwa.

“Serikali imeweka mkakati gani angalau kidato cha tano na sita wanatoka nje ya mazingira yao ili kuzingatia   mshikamano na umoja wa Taifa letu,”amehoji.

Akijibu swali hilo, Zainab amesema Serikali inatambua umuhimu wa Taifa na ndio maana shule za kidato cha tano na sita ni  za kitaifa.

“Ndio maana kipaumbele cha Serikali wakati huu ni kuhakikisha kuwa shule za kidato cha tano na sita zinapata miundombinu muhimu ikiwemo mabweni ili wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne waingie kwenye shule hizi za kitaifa,”amesema.

Related Posts