Simba jino kwa jino na Azam FC, zatofautiana idadi ya mabao

SIMBA imeendelea kukabana koo na Azam FC ikifukuzia nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kushinda mechi yake ya mwisho ugenini msimu huu dhidi ya Dodoma Jiji kwa bao 1-0.

Bao la mshambuliaji Fredy Kouablan katika dakika ya saba limetosha kuihakikishia Simba ushindi huo muhimu mbele ya Dodoma, Wekundu wa Msimbazi wakiendeleza rekodi ya ushindi mbele ya wapinzani wao hao.

Dodoma Jiji haijawahi kupata ushindi wowote mbele ya Simba tangu ipande Ligi Kuu Bara ikipoteza mechi zote nane ilizokutana na Wekundu hao.

Bao hilo la Kouablan linakuwa la sita msimu huu kwake tangu aliposajiliwa na Simba kupitia dirisha dogo la usajili lililopita, akifunga kwa shuti kali la mguu wa kulia baada ya kupokea asisti ya winga Edwin Balua ambapo Wekundu hao walitengeneza shambulizi zuri kupitia katikati ya uwanja.

Ushindi huo wa Simba unakuwa wa 18 msimu huu kwenye mechi 27 ikifikisha pointi 60 sawa na zile za Azam FC, lakini Simba inabaki katika nafasi ya tatu kwenye msimamo ikizidiwa kwa tofauti nzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Licha Simba kupata ushindi huo, ingeweza kutengeneza ushindi mkubwa zaidi endapo washambuliaji wake Koublan, Balua na Said Ntibazonkiza ‘Saido’ kama wangekuwa na utulivu kwani wamepoteza nafasi za wazi za kufunga.

Simba na Azam sasa zitaendelea kukana koo kuwania nafasi ya pili kila moja ikiitakiwa kwa kutumia mechi tatu zilizosalia kabla ya kumaliza ligi.

Related Posts