Taifa Gas waanika mikakati kupunguza gharama za gesi ya kupikia

KATIKA kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, Kampuni ya Taifa Gas imefungua maduka 250 nchini ya usambazaji wa gesi hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Pia imezindua mtungi wa kilo sita ili kurahisisha upatikanaji wa nishati hiyo kwa Watanzania wenye kipato cha chini.

Hayo yamebainishwa leo Ijumaa na Meneja Mkuu wa Taifa Gesi, Devis Deogratius wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kubainisha mkakati wa kampuni hiyo katika kupunguza gharama za upatikanaji wa gesi kwa watumiaji.

Amesema tatizo la gharama za upatikanaji wa nishati hiyo linahitaji uwekezaji ndio maana Taifa Gas ikawekeza katika ghala la kuhifadhia gesi pamoja na kujenga vituo vya kujazia gesi kwenye kila mkoa.

“Kuna maghala ya usambazaji kwenye wilaya 14. Ili kufanikisha mkakati huu tumefungua maduka 250 ya usambazaji nchi nzima na tunaendelea.

“Mwaka jana tumeshirikiana na taasisi mbalimbali za serikali ikiwamo Ewura, REA kwa kugawa mitungi 8,100. Hivyo sisi wadau tumejikita na tunaahidi kuongeza uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu ili kumfikia kila mtanzania na kumpunguzia gharama za matumizi ya nishati safi,” amesema.

Related Posts