TPDC yaingia mkataba mwingine usambazaji gesi asilia

Dar es Salaam. Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC) limesaini mkataba wa makubaliano ya uwezeshaji wa kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi na uendelezaji wa mradi mdogo wa gesi kimiminika (Mini LNG), itakayosambazwa mbali na maeneo yaliyopita mabomba ya gesi.

Makubaliano ya ubia uliyoingiwa leo Mei 17, 2024  kati ya TPDC, Rosetta na Africa 50 kwa uwekezaji katika mradi wa Mini LNG utaleta suluhu ya ufikishaji gesi asili katika maeneo ambayo bomba la nishati hiyo bado haijafika.

Hatua hiyo ya TPDC imekuja ikiwa ni siku tisa tangu Rais Samia Suluhu Hassan azindue  mkakati wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa lengo la kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2033.

Ndani ya mkakati huo ambao ni wa miaka 10, Rais Samia anataka kuwepo nguvu ya pamoja kuanzia wahisani wa kimaendeleo, taasisi za umma na sekta binafsi ili kuongeza chachu kufikia malengo yake.

Akizungumza jijini Dar es Salaam baada ya kuingia mkataba huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC,  Mussa Makame amesema kumekuwa na changamoto ya kufikisha gesi  asilia iliyoshindiliwa (CNG) na gesi asilia inayopita kwenye mabomba katika maeneo ya mbali, kwa sababu ya kukosekana kwa uwekezaji mkubwa ambao ungesambaza gesi nchi nzima.

“CNG unapoipeleka mbali zaidi ya kilomita 400 au 500 kiuchumi bei ambayo unakwenda kuuza inakaribia gharama ya kueneza,  ili kuitatua changamoto ya kutoeneza mabomba nchi nzima tumeamua kuingia makubaliano na wenzetu,”amesema Makame.

Katika utekelezaji wa mradi huo amesema utakuwa wa mafanikio hautahakikisha tu upatikanaji wa mapema wa gesi asilia kwa viwanda, kaya na magari bali utatangaza enzi mpya ya ufanisi wa nishati na uendelevu  wa matumaini makubwa  kwa sekta ya nishati nchini.

Hata hivyo, huo unakuwa mkataba wa pili kusainiwa kati ya TPDC na wawekezaji binafsi kwa ajili ya uwekezaji katika mradi wa Mini LNG baada ya ule uliotiwa saini Januari 2024 na KS Energy.

Kaimu Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi TPDC, Paul Makanza  amesema  kusainiwa kwa makubaliano hayo ni hatua muhimu kwani inaendana na mipango yao ya kuongeza usambazaji wa gesi asilia kufikia mikoa mingi hapa nchini.

“Mradi wa Mini LNG sio tu unakuza ukuaji wa viwanda lakini pia unaleta manufaa ya kiuchumi kwa jamii kupunguza gharama za uzalishaji wa gesi asilia, ikiwa ni vyanzo bora vya nishati inayotumika katika tasnia ya utengenezaji, itachangia ukuaji na ustawi wa Taifa letu,”amesema.

Amesema jukumu lao ni kuhakikisha upatikanaji wa kutosha wa gesi asilia ambapo ni muhimu kwa uendelevu wa mradi lakini pia kwa usalama wa nishati ya Taifa na uzalishaji mpya unatarajiwa katika uwanja wa Ntorya ifikapo 2025/2026, na hivyo kuimarisha hifadhi za nishati.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Rosetta Ernegy Solution, Karim Shaaban amesema kuingia mkataba huo ni katika kuunga mkono dira ya nchi katika kuwezesha usalama wa nishati kwa Taifa kwa bei nafuu na shindani.

Pia, amesema uwekezaji huo utagharimu  zaidi ya Dola milioni 100, na unalenga kuhamisha maarifa na ustawi wao kwenye soko la kutengeneza msururu wa ajira nchini,  na kuwa wachangiaji wakubwa wa pato la ndani la Taifa.

Related Posts