Dar es Salaam. Hali imeendelea kuwa ngumu katika ufaulu wa mtihani wa leseni ya Baraza la Famasia Tanzania kada ya watoa dawa na fundi dawa wasaidizi, baada ya robo tatu ya wanafunzi kufeli.
Katika mtihani huo uliohusisha watahiniwa 200, wanafunzi 184 wameshindwa kufaulu katika awamu ya kwanza, hivyo baadhi yao wametakiwa kurudia mtihani huku wengine wakitakiwa kurudia darasa.
Hii si mara ya kwanza ufaulu duni kushuhudiwa katika mtihani wa kada hizo, iliwahi kutokea katika matokeo ya Oktoba mwaka jana, ambapo asilimia 61.2 walilazimika kurudia mtihani na wengine asilimia 23.3 wakirudia darasa.
Hali mbaya ya ufaulu ilitokea hata katika mtihani wa Aprili mwaka jana, kati ya watahiniwa 1,618 ni 514 pekee ndiyo waliofaulu, wengine waliangukia kurudia mitihani na baadhi kurudia darasa.
Taarifa ya matokeo hayo, imetolewa leo Ijumaa Mei 17, 2024 na Baraza la Famasia Tanzania, ikionyesha mwendelezo wa anguko la ufaulu wa wanafunzi katika mtihani huo.
Katika taarifa hiyo, wanafunzi 49 wa kada ya watoa dawa waliofanya mtihani huo, ni watatu pekee ndiyo waliofaulu, 35 wakitakiwa kurudia mtihani na 11 wamefeli kabisa.
Kwa upande wa kada ya fundi dawa saidizi iliyokuwa na watahiniwa 151, waliofaulu ni 13, wengine 105 wametakiwa kurudia mtihani na33 wakifeli kabisa.
Sambamba na ufaulu duni, matokeo ya mtihani wa fundi dawa sanifu yamefutwa kutokana na udanganyifu.
Hatua ya kufutwa kwa matokeo hayo, imetokana na kile kilichoelezwa na baraza hilo kuwa, ilithibitika kufanyika udanganyifu katika mitihani yote mitatu baada ya kikao cha baraza cha Mei 11.
“Matokeo hayo yamefutwa kwa mujibu wa kanuni Na. 31(2) (a) ya kanuni ya elimu na mafunzo (The pharmacy (Education and Training Regulations), 2005 G.N. No. 333 ya 2005 na Sehemu ya 11 (c) ya Mwongozo wa Mitihani ya Taaluma na Usajili,” imeeleza taarifa ya baraza hilo.
Msingi wa hatua hiyo, ni kile kilichoelezwa na baraza hilo kuwa, linalenga kuwa na wanataaluma wenye sifa na weledi, kulinda afya na usalama wa wagonjwa.
Hata hivyo, imeelezwa wanafunzi waliofutiwa matokeo hayo, wanapaswa kurudia mitihani hiyo Julai 16 hadi 18, mwaka huu bila malipo.
“Vituo vya mitihani vitakuwa kama walivyopangiwa hapo awali na namba mpya za mitihani watatumiwa hivyo hawatahitajika kujisajili tena kwenye mfumo,” limeeleza baraza hilo.
Kutokana na matokeo hayo, Sylvester Maxwell kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X ameandika tatizo ni wanaodahiliwa kusoma fani hiyo na nyingine hawana uwezo.
Nyombi naye kupitia mtandao huo, ameandika “kutokana na upungufu mkubwa wa wataalamu wa afya ‘focus’ imekuwa kwenye namba (quantity), sasa ni muhimu kuweka msisitizo kwenye ubora (quality). Hii ni changamoto mtambuka.”