Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jafo amesema jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kubeba ajenda ya nishati safi ya kupikia, zimeendelea kuzaa matunda baada ya Serikali ya Uingereza kuthibitisha kuipatia Tanzania dola za Marekani milioni 1.8 (Sh 8.8 bilioni) ili kutimiza malengo ya ajenda hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Pia amesema Rais Samia ambaye alikuwa Mwenyekiti mwenza wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Nishati Safi ya Kupikia Afrika, amefanikisha kupatikana Dola za Marekani bilioni 2.2 ilihali mkutano huo ulikuwa umelenga kukusanya dola za Marekani bilioni mbili.
Jafo amebainisha hayo leo Ijumaa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu yaliyojiri katika mkutano huo uliofanyika tarehe 14 Mei mwaka huu jijini Paris nchini Ufaransa.
Amesema mkakati wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia uliozinduliwa hivi karibuni na Rais Samia, unahitaji dola za Marekani 1.8 bilioni hivyo katika fedha zinazopatikana kwenye mkutano huo, pia Tanzania itapata mgawo.
Aidha, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Zuhura Yunus amesema zaidi ya watu 1000 walihudhuria mkutano huo, ukihusisha marais, mawaziri wakuu, watu mashuhuri na wadau wa maendeleo.
Amesema malengo ya mkutano huo yalilenga kuhakikisha anga za kimataifa zinatoa kipaumbele kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, uwepo na sera za nishati safi ya kupikia kwa nchi ambazo bado zinasuasua na kuharakisha ushirikiano wa wadau mbalimbali kuhusu ajenda za nishati safi.
“Taasisi ya kimataifa ya nishati (IEA) inakadiria kuwa uwekezaji wa dola za Marekani bilioni nne unahitaji kila mwaka kwa Bara la Afrika ili watu wote waweze kutumia nsihati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2030.
“Mkutano wa 28 wa kila mwaka wa Umoja wa Mataifa (UN) wa mabadiliko ya tabia nchi (COP28) uliofanyika Novemba mwaka jana huko Dubai ndio alizindua mpango wa nishati hivyo huu ni mwendelezo kupeleka kwenye nchi za kimataifa.
Amesema mafanikio yaliyopatikana katika mkutano huo ni pamoja na ahadi serikali mbalimbali zilitolewa, washirika wa maendeleo na sekta binafsi ambazo zimeahidi kukusanya dola za Marekani 2.2 bilioni.
“Pia Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) imeahidi kutoa Dola za Marekani bilioni mbili kwa kipindi cha miaka 10. Nchi, mashirika na makampuni 132 zimeidhinisha tamko la viongozi wa juu kuhusu suala kutoa kipaumbele kwa nishati safi ya kupikia.
“Kutokana na jitihada hizi za Rais Samia kufanikisha mkutano huu, Rais wa AFDB, Dk. Akinumwi Adesina naye amesema Rais Samia amedhihirisha kuwa ni kiongozi mahiri wa Afrika wa kumuenzi kwani amekuwa na ushawishi mkubwa wa kimataifa,” amesema.
Aidha, amesema kando ya mkutano huo, Rais Samia pia aliteta na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron na kuzungumzia zaidi umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kwenye nishatti safi, maji, uwezeshaji wanawake, kilimo, biashara na uwekezaji, miundombinu, amani na usalama kaskazini mwa Msumbiji na DRC Congo.