VIDEO: Dakika 90 za hekaheka kufungwa Barabara ya Kilwa

Dar es Salaam. Ni hekaheka katika Barabara ya Kilwa inayounganisha Jiji la Dar es Salaam na mikoa ya kusini, kutokana na wakazi wa Mtaa wa Kimbangulile kuifunga kwa takribani dakika 90 wakidai kuchoshwa na ajali zinazotokea kila uchwao.

Hatua hiyo imetokana na ajali iliyotokea jioni ya jana Mei 16, 2024 iliyosababisha vifo vya watu wanne waliokuwa wakipita pembezoni mwa daraja lililopo eneo la Mto Mzinga.

Walioshuhudia wameeleza ajali ilitokea baada ya gari lililokuwa na mzigo wa maji, kumshinda dereva, ambaye katika jitihada za kukwepa magari mengine aliwagonga  watembea kwa miguu na watu wengine waliokuwa kwenye bodaboda. Gari hilo baadaye lilitumbukia mtoni.

Kuhusu kufunga barabara, wakazi hao wamesema wamefikia uamuzi huo kwa sababu wamechoshwa kushuhudia vifo vinavyotokea eneo hilo, huku watoto wao wakiwa hatarini zaidi.

Mapema leo Mei 17, 2024 saa 12.45 asubuhi Mwananchi Digital imeshuhudia kundi la wanawake wakihamasishana kukusanya mawe na magogo ambayo waliyaweka katikati ya barabara kuzuia magari yasipite.

Haikuwa rahisi kwao kufanikisha azma hiyo kwa sababu walikabiliana na upinzani kutoka kwa madereva, hasa wa bodaboda lakini kadiri muda ulivyosonga waliwazidi nguvu, hapakuwa na gari wala pikipiki iliyopita eneo hilo.

Watumiaji wa Barabara ya Kilwa wakakumbana na adha ya kufungwa barabara hiyo.


Wananchi Mbagala wafunga barabara kisa ajali

Fatma Ndembo, mkazi wa Mzinga amesema wameamua kufunga barabara ili kuzikumbusha mamlaka umuhimu wa kuifanyia upanuzi barabara hiyo ili kuwanusuru na ajali zinazotokea kila siku.

“Barabara hii ni nyembamba, hapa kwenye daraja hakuna sehemu ya watembea kwa miguu, iliyopo imeshaoza watu wanaogopa kupita, hivyo tunashindana na magari barabarani matokeo yake ndiyo haya,” amesema.

“Hapa kila siku ni ajali, nimeshazika watoto wawili, mtaani tumeshapoteza watu wengi kwa sababu ya barabara hii, sasa tunataka wahusika waone na wajue tumechoka,” amesema Fatma huku akiangua kilio.

Si kwa Fatma pekee, Salum Rashid ametokwa machozi akieleza kuumizwa na mfululizo wa ajali zinazogharimu maisha ya watu wengi wasio na hatia.

“Haturidhishwi na hiki kinachoendelea, tunataka huu mlima uchongwe, ipatikane njia, pia hapa darajani itengenezwe sehemu ya wapita kwa miguu hatuna amani watoto wetu wanagongwa kila siku,” amesema Rashid.

Ilikuwa dakika 90 za mateso kwa abiria waliokuwa kwenye mabasi yaliyokuwa safarini kuelekea mikoa ya kusini na wale waliokuwa wakienda kwenye shughuli zao.

Hata hivyo, baadhi ya watumiaji wa barabara hiyo wamepongeza hatua iliyochukuliwa na wakazi hao wakieleza ipo haja kwa Serikali kuiangalia barabara hiyo muhimu inayounganisha Dar es Salaam na mikoa ya kusini.

“Ni kweli shughuli zimesimama na tunachelewa kwenye majukumu yetu ila naona walichofanya ni sawa tu, barabara hii imeshakuwa tatizo sugu, foleni na ajali kila siku,” amesema Mariam Sefu.

Barabara iliendelea kufungwa hadi saa mbili kamili polisi walipofika eneo la tukio na kufungua njia.

Related Posts