Waliovamia mlima Kawetere wamilikishwa hekari nyingine 698

Mbeya. Serikali kupitia Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) imetoa eneo lenye ukubwa wa hekari 698 kwa wananchi wanaodaiwa kuvamia hifadhi ya Mlima Kawetere na kujenga makazi ya kudumu kinyume cha sheria.

Hatua  hiyo imetokana na agizo la Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera kutaka busara itumike baada ya kuwepo kwa mvutano wa wananchi wa vijiji vya Ruiwa wilayani Mbarali na Malamba Kata ya Itezi Wilaya ya Mbeya na TFS uliodumu kwa kipindi kirefu licha ya kuwekwa mipaka.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Mei 17, 2024 Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amesema jana Mei 16, 2024 yeye na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Denis Mwila walifika katika vijiji hivyo na kuzungumza na wananchi kuhusiana na mvutano huo, kisha wakawaeleza kile walichoagizwa na Serikali ya mkoa kupitia kwa mkuu wa mkoa huo, Homera,

Malisa amesema wananchi waliovamia maeneo ya hifadhi kwa kujenga  makazi  na shughuli za kilimo waliopaswa kuondoka sasa Serikali imeagiza TFS itenge maeneo zaidi kwa ajili yao.

“Na mimi tayari nimeshauagiza uongozi wa TFS kuanza kuweka mipaka kwa kushirikisha na jamii ya maeneo husika, ili kuondoa migogoro kwa siku za  mbeleni,” amesema Malisa.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali Mwila alisema kadri siku zinavyozidi kwenda ndivyo wananchi wanavyoendelea kujimilikisha maeneo katika hifadhi ya mlima huo unaosimamiwa na TFS.

Amesema kama Serikali isingechukua hatua, huenda msitu huo ungeteketea na kusababisha madhara makubwa zaidi yakiwamo ya ukame katika maeneo hayo.

“Ili kuepuka madhara kama ya ukosefu wa mvua na ukame, Serikali imelazimika kuingilia kati kwa kuwaondoa watu wote waliojenga makazi ndani ya hifadhi kwa lengo la kulinda rasilimali za miti na ikolojia ya mlima Kawetere,” amesema mkuu huyo wa mkoa.

Hata hivyo, kutokana na agizo la Mkuu wa Mkoa, tayari wataalamu wa ardhi wameshafanya tathimini ya kuainisha maeneo ambayo hayataruhusiwa kwa kilimo na mengine yatabaki chini ya hifadhi kwa utaratibu maalumu utakaowekwa.

“Katika utengwaji wa maeneo, baadhi ya mashamba ya wananchi yatamegwa na kurejeshwa hifadhini na wale ambao wameingia ndani zaidi ya hifadhi, wataondolewa na kusogezwa kule kuliko tengwa ardhi kwa ajili yao,” amesema.

Kwa upande wake, Ofisa Misitu wa TFS, Isdor Chuwa amesema tayari wametenga eneo lenye ukubwa wa hekari 698 ambazo watagawiwa wananchi hususan wale waliokuwa wakilima jirani kabisa na hifadhi ya mlima.

“Wananchi waliokuwa wanaishi ndani ya hifadhi ni wavamizi ambao watapaswa kuondolewa kwa mujibu wa sheria, lakini tunafuata  busara za viongozi kama walivyotuagiza, tutawapatia maeneo mengine,” amesema Chuwa.

Mkazi wa kijiji cha Ruiwan, Edina Julias amesema licha ya Serikali kutamka kuwa watapatiwa ardhi nyingine, bado wana hofu kwa sababu wameishi maeneo hayo kwa miaka mingi, huko wanakopelekwa wanaenda kuanza maisha upya.

Naye mkazi wa Malamba, Kenedy Mwailamba ameishukuru Serikali kwa hatua ya kutafuta suluhisho ya mgogoro huo uliodumu kwa miaka mingi.

“Nadhani sasa hata yale mapigano ya askari wa hifadhi na wananchi yataisha, cha msingi ni wananchi kukubali kuondoka kwa sababu wamepewa ardhi nyingine,” amesema Mwailamba.

Related Posts