Wanaume 17, 694 washiriki kupeleka wake zao kliniki

Unguja. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema kuwa kinababa 17,694 sawa na asilimia 34 ya kinamama wote waliokwenda kliniki ya afya ya uzazi na mtoto walishiriki  kuwapeleka wenza wao kupata huduma za afya ya uzazi na mtoto wakati wa ujauzito.

Hayo yamebainika leo Mei 17, 2024 katika mkutano wa 15 wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Unguja, Zanzibar na Naibu Waziri wa Afya, Hassan Hafidh alipokuwa akijibu swali la Mwakilishi wa Mwanakwerekwe,  Ameir Abdalla Ameir aliyetaka kujua tathmini iko vipi juu ya ushiriki wa wanaume katika huduma za afya ya uzazi pamoja na huduma za uzazi wa mpango.

Hafidh amesema kwa mujibu wa takwimu za vituo vya afya na hospitali kwa Unguja na Pemba, kinababa 17,694 sawa na asilimia 34 ya kinamama wote waliokwenda kliniki ya afya ya uzazi na mtoto walishiriki kwa kuwapeleka wenza wao kwa ajili ya kupata huduma za afya ya uzazi na mtoto wakati wa ujauzito.

Takwimu hizo ni kwa kipindi cha kuanzia Julai 2023 hadi Machi 2024.

Vilevile kwa upande wa huduma za uzazi wa mpango jumla ya kinababa 539 walipatiwa njia ya uzazi wa mpango (Kondomu) katika vituo mbalimbali vya afya kwa Unguja na Pemba.

Katika hatua nyingine imesajili taasisi zisizo za kiserikali 2,713 ambazo zinatoa huduma na misaada mbalimbali ili kuleta ustawi katika jamii.

Akizungumza leo Mei 17, 2024 katika mkutano wa 15 wa Baraza la wawakilishi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ,  Masoud Muhammed alipokuwa akijibu swali la mwakilishi wa Mwanakwerekwe Ameir, aliyetaka kujua ni taasisi ngapi zisizo za kiserikali zimesajiliwa kihalali hadi kufikia sasa.

Pia, alitaka kujua ni taasisi gani kati ya hizo ambazo zina malengo mahususi ya kuulinda na kuudumisha utamaduni wa Mzanzibari.

Waziri Masoud amesema SMZ  kupitia Ofisi ya Msajili wa Jumuiya zisizo za Kiserkali (NGO) hadi kufikia Machi, 2024 tayari imeshazisajili NGO 2,713.

Amesema NGO hizo zina lengo kuu la kutoa misaada mbalimbali kwa jamii kutegemeana na jumuiya husika ili kuleta ustawi.

“Kwa mantiki hiyo, hakuna Jumuiya iliyojisajili mahususi kwa lengo la kuulinda na kuudumisha utamaduni wa Mzanzibari,” amesema.

Hata hivyo Masoud amesema kwa kuwa NGO  huundwa na wageni pamoja na wananchi,  hivyo zina wajibu wa kufuata taratibu na sheria za nchi ikiwemo suala zima la kuulinda utamaduni, mila na desturi.

Kuhusu tathmini ya utendaji wa taasisi hizo, Waziri Masoud amesema inaonyesha ziko vizuri  kwa vile zimekuwa zikisaidia katika kukuza sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii kama vile afya, elimu, barabara, mazingira, maji na kilimo.

Related Posts