ANTI BETTIE: Usitafute maisha ukasahau kuishi, acha kulalamika

Nilifunga ndoa na mwenza wangu miaka sita iliyopita. Wakati huo ndiyo kwanza alikuwa ameanza kazi, kwa juhudi zake na elimu aliyonayo amepanda vyeo na sasa ni mtu mkubwa tu anapofanyia kazi.

Changamoto yake ana matumizi mabaya ya fedha hasa unapofika mwisho wa mwaka. Licha ya kuwa na imani ya dini, mapenzi, kutunza familia vema hili linanikera sana.

Kila unapofika mwisho wa mwaka anatumia zaidi ya Sh10 milioni kwa ajili ya kututembeza huku na kule, mwenyewe anasema kufurahia maisha. Huwa ninakwenda kumridhisha, lakini fedha zinazotumika ninawaza tungekuwa tunawekeza naamini tungekuwa mbali zaidi ya hapa tulipo sasa. Nishauri nifanyeje aachane na haya matumizi mabaya ya fedha.

… Mmh! Yanaweza kuwa matumizi mabaya ya fedha au yasiwe kulingana na anachokiingiza kwa mwaka na lengo la kuwapeleka huko mnakokwendaga kama mwenyewe anavyosema kufurahia maisha.

Sijui vizuri kuhusu uwekezaji alioufanya mpaka sasa na matumizi ya hizo fedha, ila ninachojua anatoka na familia yake kwenda kuupa mwili shukurani kwa kazi uliyofanya mwaka mzima kutafuta fedha, tena akiwa na familia yake. Hili kwanza liheshimiwe, wengine huwa wanakwenda na marafiki.

Tulio wengi tunatafuta maisha na kusahau kuishi, kuna wakati lazima uishi kwa sababu maisha yenyewe ndiyo haya haya, ilimradi hafanyi vitu tofauti kama ulevi na marafiki, kuhonga wanaume, bali anaikusanya familia yake huyu ni wa maana sana.

Punguza kulalamika kuishi, kufurahi ni sehemu ya maisha upe mwili pole siku moja moja kama anavyofanya mwenza wako, mnatafuta pesa mwaka mzima kuzitumia kwa nini iwe shida. Kama hajawekeza mshauri kufanya hivyo, lakini hilo lisiwanyime fursa ya kuupa mwili pole, unachoweza kufanya ni kuhakikisha anapunguza kiwango cha pesa mnazotumia, lakini siyo kuacha kabisa kuupoza mwili baada ya pirikapirika za mwaka mzima.

Mtoto ameniondoa chumbani kwangu

Anti nipongeze kwanza kwa kupata mtoto, kisha nipe pole kwani ameniondoa chumbani kwangu, eneo ambalo nilikuwa nikikutana na mke wangu, yaani mama yake.

Mke wangu anajua mapenzi na kubembeleza, ndiyo maana nilikuwa ninapenda sana kukaa naye chumbani, hata taarifa ya habari, magazeti na movie nilikuwa nikitazamia huko. Lakini sasa huyu mtoto ameniondoa kabisa kwenye kuti langu la mazoea, kwani hata nikiwa huko na mama yake hanioni anakuwa bize na mwanaye (mtoto wetu mpenzi).

Nauliza kuzaa kuna uhusiano na mapenzi ya wenza kupungua? Je, nifanyeje kuyarudisha?

 …Pole sana. Wanawake mnawakosea wenza wenu, unahamishiaje mapenzi kwa mtoto na kumsahau aliyekupa huyo mtoto? Bila mapenzi angepatikana kweli?

Mnawanyima raha wenza wenu bila sababu eti! Imekuwa ni desturi mwanamke aliyezaa kuchukia kukutana kimwili na mwenza wake.

Wengine hata mabusu hawapigani tena, kutwa na mtoto begani, mikononi.

Mbali na hilo hata mapenzi pia mnahamishia kwa mtoto na kuwasahau wenza wenu mnaoishi nao nyumba moja.

Simaanishi muwachukie watoto, lakini hilo halina uhusiano na kuwaweka mbali wenza wenu, au mmesahau kuwa bila wao hao watoto msingewapata.

Kuzaa, kulea hakuna uhusiano na kuguna, kukataa, kutoa kwa shingo upande mapenzi kwa mumeo au mwenza wako hususani mapenzi ya faragha, kujamiiana, kuingiliana kimwili.

Hii imekuwa karaha kubwa miongoni mwa wanawake hususani walioolewa, mnaona sifa eeh…nauliza kumnyima mumeo au mwenza wako unyumba ni sifa au kashifa unajikashifu mwenyewe kwa kushindwa kutimiza majukumu yako ya msingi.

Kibaya zaidi kabla hamjazaa mlikuwa mnawajali wanaume wenu kwa kuwapikia vizuri, kuwapokea wakitoka kazini, kuwabusu wanapoondoka asubuhi hata kama mnaongozana wote na kuwaandalia mavazi.

Lakini wakitaka huduma hizo sasa mnakasirika na kujifanya kama mmezaa dunia.

Watoto wana nafasi yao na mume, mwenza, mpenzi ana nafasi yake na hilo lipo tangu enzi na enzi, anayeshindwa kujigawa hawezi kuwa mwanamke labda kitu kingine.

….Nina kazi nyingi baba fulani naye akija atataka nimkorogee kahawa, hafikirii jinsi mtoto alivyonisumbua kutwa nzima!

Anayetoa kauli hizi amepoteza sifa ya kuwa mwanamke, mpenzi, mke au mwenza wa mtu. Mwenye sifa hizo anatakiwa kujipanga na kila mtu kumpa nafasi yake anayostahili.

Unajua kama chanzo cha furaha kwa wanaume ni pamoja na kujamiiana.

Sasa wewe mpe kama unamuonjesha asali kwanza ang’atwe na nyuki ndiyo apate utamu, wenzako watampa kabla hajaomba.

Vitu vingine viwashinde wanakwetu basi hata hili mlilo na asili nalo la kumuhudumia bwana liwashinde, kitu chenyewe kipo kwa ajili ya kazi hiyo nyingine ni za ziada, usipokitumia kwa kazi hiyo unataka ukifanyie nini.

Kuzaa, kuwa na mtoto mlizi na mkorofi kusikufanye umkimbie mumeo, mjumuishe mkabiliane na hatua za makuzi ya mtoto wenu huku mkiendeleza huba lenu kama kawaida.

Kweli kuna baadhi ya vitu vitapungua ikiwamo mtoto kuwapangia muda , maana mtamsubiri mpaka alale, lakini hicho siyo kikwazo.

Related Posts