Faru waliotoweka kwa miaka 30 kurejeshwa Hifadhi ya Mikumi

Morogoro. Baada ya faru weusi kutoweka kwa zaidi ya miaka 30 iliyopita kutokana na kuuawa na majangili, Serikali kupitia Hifadhi za Taifa (Tanapa), imeanza mchakato wa kuwarejesha katika Hifadhi ya Mikumi.

Faru weusi wako kwenye orodha ya wanyama walio hatarini kutoweka duniani huku Tanzania kupitia mpango wa Taifa wa miaka mitano wa uhifadhi wa faru weusi imeendelea kuwatunza 100 waliokuwepo tangu mwaka 1990 ambao sasa wamefikia 238.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Jumamosi, Mei 18, 2024, Ofisa Uhifadhi Daraja la Pili Kitengo cha Uhusiano wa Jamii wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, David Kadomo amesema wakati hifadhi hiyo inaadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1964, wanatarajia kukamilisha mradi wa urejeshaji wa faru weusi kwa ajili ya kuongeza idadi ya watalii na pato la Taifa.

Amesema tayari wameshafanya utambuzi wa eneo watakalowaweka na wanachosubiri ni upatikanaji wa fedha kwa mwaka huu wa 2024/2025 kwa ajili ya kuanza kuwahamisha.

“Tunasubiri fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huu, tutawahamisha kutoka hifadhi za hapa nchini lakini wengine kutoka Afrika Kusini sambamba na kuimarisha ulinzi wao,” amesema Kadomo.

Hifadhi ya Taifa ya Mikumi iliyoko Mkoa wa  Morogoro ni moja ya zilizoathirika na ujangili wa faru.

Mratibu wa Faru kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Philibert Ngoti amesema kwa kipindi cha kuanzia mwaka 1970 hadi 1980, Tanzania ilikuwa na faru weusi 10,000 hali iliyoifanya ijulikane duniani kuwa miongoni mwa nchi zenye wanyama hao wengi barani Afrika. “Mwanzoni mwa miaka ya 1980 hadi 1990 idadi ya faru ilipungua sana na kuwa chini ya 100, kutokana na uwindaji haramu na kusababisha upungufu mkubwa wa faru katika nchi zote zenye faru barani Afrika na kuwekwa kwenye kundi la wanyama walio hatarini kutoweka duniani,” amesema.

Amesema katika kunusuru hilo, mwaka 1993 Serikali ilikuja na toleo la kwanza la mpango wa Taifa wa miaka mitano la Uhifadhi wa Faru Weusi lilihuishwa hadi ilipofikia tamati 2023 na sasa Tanzania ina utajiri mkubwa wa faru hasa katika hifadhi za Burigi-Chato, Serengeti na Mkomazi.

Akizungumzia hilo, Ofisa Uhifadhi Daraja la Pili, Kitengo cha Uhusiano wa Jamii katika Hifadhi ya Mikumi, Emakulata Mbawi amesema katika kuhakikisha usalama wa mazao ya hifadhi ikiwamo wanyamapori inakuwa salama, wameweka ukaribu na wananchi wa vijiji 13 vinavyowazunguka kutoka wilaya tatu za Mogorogo, Kilosa na Mvomero wanaosaidia uhifadhi.

“Mazao ya hifadhi wakiwamo wanyamapori kwa sasa wako salama kutokana na miradi ya ujirani mwema tuliyonayo baina yetu na wananchi, hivyo hata huo mradi wa Faru utakapofika tunaamini watakuwa sehemu salama,” amesema.

Related Posts