Dar es Salaam. Wakati Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ikipitisha kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za mwaka 2024 na kanuni za uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura za mwaka 2024, baadhi ya vyama na asasi za kiraia zimelalamika kutopewa muda wa kutosha kuzipitia, hivyo kushindwa kutoa mapendekezo.
Kanuni hizo zinalenga kutafsiri sheria zilizotungwa na Bunge zinazohusu uchaguzi, ambazo ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024 na Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya mwaka 2024.
Taarifa ya kupitishwa kwa kanuni hizo ilitangazwa kupitia mitandao ya kijamii, ukiwamo wa X, baada ya kikao kilichofanyika Mjini Unguja, Zanzibar Mei 11, 2024.
Taarifa hiyo imesema baada ya kupitishwa kwa kanuni hizo, hatua inayofuata ni kuzichapisha kwenye gazeti la Serikali Mei 17, 2024 ili ziweze kutumika rasmi.
“Kanuni hizo zimepitishwa baada ya kuandaliwa na wataalamu na kupelekwa kwa wadau kwa ajili ya kutoa maoni yao ambayo yamefanyiwa kazi na kujumuishwa,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi, baadhi ya wadau wamelalamika kutopewa muda wa kutosha, jambo ambalo hata hivyo limekanwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima, akisema muda uliotolewa unatosha na kwamba hakuna utaratibu wa wadau kuitwa kuwasilisha maoni.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Itifaki, Uhusiano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema walipokea barua pamoja na barua pepe kutoka INEC ikiwataka watoe maoni kuhusu kanuni hizo na walijibu.
“Sisi tulipewa siku saba na tumewajibu, nadhani wanaangalia kila chama na utaratibu wake,” amesema.
Mkurugenzi wa Uhusiano wa CUF, Mohamed Ngulangwa amesema hawakutoa maoni kwa kuwa walipewa siku nne pekee.
“Walitoa kanuni Aprili 15 na mwisho uwe Aprili 19, 2024. Ukipima mtu mwenye hila utaona kabisa. Huwezi ukatoa document (waraka) yenye kurasa zaidi ya 100 halafu utoe maoni kwa muda huo.”
“Kwa vyama vikubwa vinavyoongozwa kitaasisi, hatoi maoni mtu mmoja, ni lazima uitishe mkutano. Labda kwa vyama vidogo, lakini muda haukutosha kuchambua nyaraka yenye zaidi ya kurasa 100, kwa hiyo tuliwapa viongozi na kama wametoa maoni ni ya kirafiki, siyo ya kitaasisi,” amesema Ngulangwa.
Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amesema: “Tume imepitia hatua muhimu ya kuwashirikisha wadau. Walitutumia kanuni kwa barua pepe kwa siku chache na utaratibu tunaoujua ni kwamba, tukishafanya uchambuzi wetu huwa tunaitwa na tume kuwasilisha na kupewa uelewa, lakini mwaka huu jambo hilo halikufanyika.”
Amesema baada ya kanuni hizo kuletwa na INEC walishaanza maandalizi ya kuzichambua, lakini wakasikia zimepitishwa.
Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe amesema hawajaziona kabisa kanuni hizo.
Malalamiko ya muda pia yametolewa na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), huku Kaimu Mkurugenzi wake, Mackphason Mshana, akisema wao hawakutoa maoni kabisa.
“Hatukutoa maoni kwa sababu muda ulikuwa umeisha, wakati tunaendelea kuchambua tukasikia Tume wameshatoa kanuni. Sisi huwa tuna kamati ya wanasheria na wajumbe wake wana kazi zao, hivyo ni lazima watafutwe. Pia huwa tunapenda wanachama wetu pia watoe maoni yapelekwe kwenye kamati,” amesema.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga amesema: “Tulipewa kanuni, lakini hatukupewa deadline (makataa), kabla ya kukamilisha uchambuzi, tunasikia zimeshatangazwa.
“Haikuzidi siku mbili, yaani kama leo tumepata, kesho tunaanza kujadili, jioni tunasikia zimeshapitishwa,” amesema.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Kailima akijibu malalamiko hayo, amesema muda uliotolewa unatosha na hakuna utaratibu wa wadau kuitwa kuwasilisha maoni.
“Tangu lini tukawaita kuwasilisha maoni yao, huu siyo uchaguzi wa Serikali za Mitaa,” amesema Kailima.
“Katika vyama vya siasa 19, vyama 16 wamewasilisha maoni, hao kina nani ambao hawajawasilisha? Wao kama hawajawasilisha ni hiari yao, hao 16 wamepata muda upi kuwasilisha?”
Kailima aliendelea kusema: “Wadau 104 tumepokea maoni yao, hao nao wamepata muda upi? Wadau hao wametoa maoni na tumeyafanyia kazi.”.
Amesema kanuni hizo zitachapishwa kuanzia Jumatatu Mei 20, 2024 kwenye tovuti ya INEC.