Ken Gold yataka mastaa wa Ligi Kuu

Ken Gold imesema itakuwa makini kufuatilia mechi zilizobaki za Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA) ili kupata wachezaji watakaojumuishwa katika kikosi cha timu hiyo msimu ujao.

Pia imesisitiza kuwa siyo kwa timu kubwa za Simba na Yanga, bali hata nyingine zinazocheza Ligi Kuu ikiwamo KMC, Coastal Union, Prisons na Ihefu itazifuatilia ili kuhakikisha inakuwa na kikosi bora cha kushindana msimu ujao.

Ken Gold ya wilayani Chunya mkoani Mbeya inajiandaa na Ligi Kuu ikitarajia kushiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo baada ya kupanda daraja huku ikimaliza Championship kinara kwa pointi 71.

Katibu Mkuu wa timu hiyo, Benson Mkocha ameliambia Mwanaspoti Online kuwa wakati wakiendelea kutafuta mastaa ndani na nje, lakini wako karibu sana na Ligi Kuu ili mechi tatu zilizobaki wanazifaidi kwa kupata nyota wa kujumuishwa kikosini.

Amesema mbali na Ligi Kuu, pia mechi za nusu fainali za kombe la shirikisho wanazitupia macho kuhakikisha wanapata wachezaji ambao watakuwa bora kutoa ushindani kwa timu hiyo.

“Hatuangalii timu kubwa tu, bali hata zile nyinginezo kwa sababu wapo wachezaji wenye uwezo, hivyo baada ya msimu kuisha tutajua nani tumekubaliana naye kuitumikia Ken Gold,” amesema Mkocha.

Kuhusu benchi la ufundi, katibu huyo amesema hadi sasa wana majina matatu ya wazawa na wanasubiri wamalize mikataba ili kuanza makubaliano rasmi kuungana na wachimba madini hao.

“Kocha Mkuu atakuwa mzawa na tunayo majina matatu japokuwa ni mapema kuwataja kwakuwa bado wana mikataba yao na timu za Ligi Kuu, baada ya Mei 28 ligi kuisha tutaweka wazi” amesema.

“Kambi yetu itaanza mapema mwezi Juni ambapo tutakuwa tumeweka mipango sawa, hadi sasa wapo wachezaji tunao katika mazungumzo wakiwamo wa Ligi Kuu na wengine kutoka nje na muda wowote tutamalizana nao.”

Related Posts