Dodoma. Mawaziri na naibu mawaziri sita wamepambana kuiokoa bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu kwa mwaka 2024/25.
Walifanya kazi hiyo walipochangia na kujibu hoja za wabunge walizotoa walipochangia mjadala wa kupitisha bajeti hiyo bungeni jana.
Kwa muda mrefu bajeti zilizozoeleka kuwa na wachangiaji mawaziri na naibu mawaziri ni za Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi na Bajeti Kuu ya Serikali, lakini juzi hali ilikuwa tofauti kwa wizara hiyo.
Waliochangia ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni na Naibu waziri wa Maendeleo ya Jamii, Mwanaidi Ali Khamis na Naibu waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Ridhiwani Kikwete.
Wengine ni wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange, na wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini.
Wizara hiyo iliundwa katika mabadiliko madogo yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, Januari 8 mwaka 2022, akimteua Dk Gwajima kuwa waziri kwenye wizara hiyo, hivyo kuifanya bajeti hiyo kuwa ya tatu kwake.
Mambo yalianza kujidhihirisha mapema asubuhi, wabunge walipochangia baadhi wakihoji ni kwa vipi hotuba haionyeshi atakavyopambana na ndoa za jinsi moja, na ukatili wa kijinsia kwa watoto na vijana.
Mbunge wa Singida Kaskazini, Ramadhan Ighondo, alisema haungi mkono bajeti hiyo na kutoa wito kwa wabunge wenzake kutoiunga mkono, kwa sababu wahusika wameshindwa kuchukua hatua kuwalinda Watanzania, hasa watoto.
Alimhoji Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni kuhusu alichosema kama kigugumizi cha kuchukua hatua kwa taarifa za mambo yaliyo kinyume cha utamaduni wa Watanzania.
Mbunge wa Viti Maalumu, Mwantumu Dau Haji, alisema katika hotuba ya Dk Gwajima hakuna mustakabali wa kukomesha ubakaji na ulawiti, hivyo kushauri watakaobainika wahasiwe kwa kuchomwa sindano, kwani tatizo hilo ni kubwa.
Kwa hoja za wabunge hao na wengine waliokemea vitendo hivyo, mawaziri na naibu mawaziri walisimama kuchangia kujibu hoja zilizoibuliwa.
Naibu Waziri Sagini amesema Tume ya Marekebisho ya Sheria, imefanya uchambuzi na kubaini baadhi ya sheria ambazo zinaharamisha baadhi ya makosa ambayo wabunge wamezungumza kwa uchungu.
“Tume yetu imeenda mbali na kubaini sababu za mmomonyoko huu wa jamii ambayo moja ni mila na desturi, matumizi ya dawa za kulevya na imani za kishirikina,” amesema.
Amesema nyingine ni malezi, talaka, kazi za sanaa, vibanda umiza vinavyoonyesha picha za ngono, tabia za wazazi, malezi mabaya na ulevi.
Sababu nyingine amesema ni za kiuchumi ambazo ni umasikini uliokithiri, kukosekana kwa ajira, na za kiteknolojia ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya mitandao, simu janja na runinga.
Naibu Waziri Dugange alisema wameunda kamati maalumu 115 kuhakikisha zinafuatilia viashiria, lakini pia kukomesha ukatili wa wanawake na watoto.
“Tumehakikisha tunaelimisha kwa kutoa elimu kwa ngazi ya vijiji, mitaa, kata na kuunda kamati kwa ajili ya kufuatilia na kuchukua hatua, ikiwa ni pamoja na kufanya midahalo,” amesema.
Naibu Waziri Kikwete amesema changamoto ya maofisa maendeleo ya jamii wanaenda kuifanyia kazi.
Amesema ndani ya kipindi cha miaka miwili, zaidi ya maofisa maendeleo ya jamii 2,140 waliajiriwa, akisema pia wameajiri maofisa ustawi wa jamii 403 katika mwaka 2023/24.
Alisema mwaka 2024/25 baada ya kilio cha wabunge wataajiri maofisa ustawi wa jamii 472.
Masauni amesema miongoni mwa hatua walizochukua ni kuwatimua nchini watu 64 na wakimbizi 41 baada ya kubainika kuwa na viashiria vya kujihusisha na masuala ya ndoa za jinsi moja.
“Kuna hatua zinaendelea katika kupambana na vita hii, niwahakikishe wananchi vita hivi ni vyetu wote. Nawashukuru na kuwapongeza kwa kuonyesha msimamo thabiti,” alisema.
Naibu waziri, Mwanaidi Ali Khamis alisema miongoni mwa hatua walizochukua ni kufuta mashirika yote yasiyo ya kiserikali na kuyasajili upya kwa kuongeza sharti la kupeleka taarifa zao.
Dk Gwajima amesema amekuwa akipambana na matukio ya ukatili wa kijinsia kwelikweli na si kimchezo-mchezo.
Amesema wamekuja na mpango mkakati wa unaoshirikisha watu wote, wakiwamo watendaji wa wilaya, kata, mitaa kwa kuhakikisha wote wanabeba ajenda hiyo kwa kuizungumzia kila mahali.
Wabunge waliendelea kumbana Dk Gwajima pale Bunge lilipokaa kama Kamati ya Bunge kwa ajili ya kupitisha kifungu kwa kifungu.
Mbunge wa Arumeru Magharibi, Noah Lembrid amesema Dk Gwajima akijibu hoja za wabunge, hakuonyesha uzito wa hoja zilizochangiwa na kwamba Serikali inachukizwa na vitendo hivyo kama ilivyokuwa kwao.
“Sijapata kauli nzuri kutoka kwa waziri akisikitika, akionyesha masikitiko yake ya kupinga na kukemea vitendo vya ukatili na ndoa za jinsi moja, mimi sitaridhika,” amesema.
Hatua hiyo ilimfanya Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga kumtaka Dk Gwajima kujaribu kurejea jambo hilo kwa masikitiko zaidi.
Baada ya kauli hiyo, akiwa ameinama na kushika mkono kichwani, Dk Gwajima amesema: “…yaani ninasikitika, moyo unaniuma, nalia silali Watanzania ni mashahidi. Nimhakikishie mbunge nimechukulia kwa uzito, nimeandika hadi nimechapa na kuchambua hoja kutoa mapambano yangu na kusema sitaki ndoa za jinsi moja.”
Akieleza hayo, alizungumza kwa kauli yenye kuonyesha kama mtu anayelia ili kumridhisha mbunge huyo.
Hata hivyo, Bunge lilipitisha Sh67.9 bilioni za bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2024/25.