Namba za Azam siku 108 bila Dube

ZIMETIMIA siku 108 ambazo ni sawa na miezi mitatu bila uwepo wa mshambuliaji Prince Dube ndani ya kikosi cha Azam FC, lakini kinachofurahisha ni Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuendelea kukimbiza tuzo ya ufungaji bora ya Ligi Kuu Bara akiwa na mabao 15 sawa na Aziz KI wa Yanga.

Mara ya mwisho kwa Dube kuitumikia Azam FC ilikuwa Februari 9, mwaka huu, kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Simba na timu yake ikaambulia sare ya kufungana bao 1-1  akiifungia timu hiyo na bao la Simba lilifungwa na Clatous Chama.

Baada ya mchezo huo mshambuliaji huyo aliripotiwa na timu yake kuwa anajiuguza majeraha hadi lilipoibuka sakata baina yake na uongozi juu ya mkataba ambalo lipo chini ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Mwanaspoti linakuletea siku 108 bila uwepo wa Dube ndani ya timu hiyo ikiwa imecheza mechi 13 imeshinda tisa, imefungwa mmoja dhidi ya Simba mabao 3-0 na sare tatu zikiwa ni takwimu za ligi pekee.

Timu hiyo bila Dube imefunga mabao 18 ilihali alipokuwepo ilikuwa imefunga 36 kwenye mechi 14 ilizocheza ndani ya ligi.

Wakati Dube mara yake ya mwisho kucheza mechi ya ligi akiwa na Azam FC ni dhidi ya Simba, timu hiyo bila mshambuliaji huyo imekubali kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Wekundu hao wa Msimbazi katika mchezo wa pili.

Kiungo Fei Toto ameendelea kupeta bila uwepo wa mshambuliaji huyo kwani tangu asepe kikosini, ametupia mabao saba kati ya 15 aliyonayo. Kuondoka kwa Dube ndani ya Azam FC kumeifanya isajili wa mastaa wawili wa kigeni kiungo Franck Tiesse kutoka Stade Malien na beki Yoro Mamadou Diaby kutoka akademi ya Yeleen Olymique ya Mali.

Pia timu hiyo imeshindwa kutamba mbele ya Simba kwenye mashindano ya Kombe la Muungano yaliyorejea mwaka huu baada ya kushinda mabao 5-2 dhidi ya KMKM na kuingia fainali, lakini ikafungwa na Simba bao 1-0 kuambulia nafasi ya pili.

Related Posts