RUWASA yachongewa, yateketeza mamilioni kwa maji yenye magadi

SAKATA la ukosefu wa maji wilayani Momba mkoani Songwe limezidi kushika kasi baada Diwani wa Kata ya Ivuna – Bonde la Kamsamba, Erick Mkamba ‘Magazeti’ kudai kuwa mamilioni fedha ya miradi ya maji iliyotolewa na Serikali, yamepotea kwa kuelekezwa kwenye miradi isiyokuwa na tija kwa wananchi. Anaripoti Ibrahim Yassin, Songwe… (endelea).

Mkamba ameyasema hayo jana Ijumaa katika mkutano wa hadhara ulioongozwa na Mkuu wa mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo kwenye kata hiyo ya Ivuna.

Amesema miradi ya maji hasa visima vilivyochimbwa na Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini (RUWASA) hayakufaa kutumiwa na binadamu kwani yana magadi kupita kiasi.

Amesema katika vitongoji 25 vya kata hiyo, ni vitongoji vitano pekee ndivyo vilivyochimbiwa visima ambavyo maji yake hayafai kwa matumizi ya binadamu licha ya mamilioni ya fedha  kutumika.

Akijibu madai hayo, Meneja wa RUWASA mkoani humo, Mhandisi Charles Pambe alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kudai kuwa baada ya maji hayo kuonekana yana chumvi nyingi, serikali imewapatia Sh 1.7 bilioni kwa ajili ya mradi mwingine wa maji.

Amesema wiki chache zijazo wakipata kibali kutoka wizarani watasaini mkataba na mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji yenye tija ambao wanaamini ndani ya miezi sita utakuwa umekamilika na wananchi kuanza kunywa maji safi.

Kutokana na maelezo hayo, Chongolo aliahidi kuwasiliana na katibu mkuu wizara ya maji kuhakikisha anatoa kibali haraka ili miradi mipya ianze kutekelezwa.

Aidha, alimtaka meneja wa Tanesco kuhakikisha anapeleka umeme kwenye vijiji hivyo ndani ya muda mfupi.

Related Posts