Sababu Songwe kuongoza mimba za utotoni

Songwe/Katavi. Mimba za utotoni ni tatizo kubwa linaloathiri jamii nyingi, hasa katika nchi zinazoendelea. Hali hii inahusisha wasichana wenye umri chini ya miaka 18 na ina athari mbaya kwa afya, elimu na maisha yao kwa ujumla.

Makala haya yanajadili sababu za mimba za utotoni, athari zake na hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kupunguza tatizo hili katika mikoa ya Songwe na Katavi ambayo imebainika kuwa na kiwango kikubwa cha mimba za utotoni.

Mimba za utotoni katika mikoa hiyo huchangiwa na sababu kadhaa zikiwamo ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi, umasikini na mila na desturi.

Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto pamoja na Viashiria vya Malaria Tanzania kwa mwaka 2022 (TDHS- MIS) unaonyesha, Tanzania imepunguza mimba za utotoni kwa asilimia tano ndani ya miaka mitano ikiwa ni sawa na asilimia moja kwa mwaka.

 Hiyo ni baada ya wastani wa mimba za utotoni kufikia asilimia 22 mwaka 2022 ikilinganishwa na asilimia 27 katika utafiti wa mwaka 2015/2016.

Ripoti inautaja Mkoa wa Songwe kuongoza kwa mimba za utoto kitaifa ukiwa na asilimia 45, Ruvuma 37, Katavi asilimia 34, Mara asilimia 31 na Rukwa asilimia 30.

Katavi inaingia kwa mara nyingine, lakini ikiwa na kiwango pungufu kutoka asilimia 45 ikilinganishwa na utafiti wa mwaka 2015-2016.

Kwa mujibu wa taarifa ya mimba za utotoni kwenye vituo vya kutokea huduma za afya kwa Aprili, 2024 mkoani Songwe kwa wajawazito chini ya miaka 18 waliohudhuria kliniki inaonyesha wapo 419.

Wilayani Ileje wapo 22 wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 17, Mbozi wapo 27 wenye umri huo.

Wilaya ya Momba wenye umri wa kati ya miaka 13-14 wako wawili, huku wenye miaka kati ya 15-17 wako 192 hivyo kufanya jumla yao kuwa 194. Wilayani Songwe wa miaka 13-14 wako tisa, huku wa miaka 15-17 wakiwa 95 na kufanya jumla kuwa 104. Wilaya ya Tunduma wapo 72 wa umri kati ya 15-17.

Ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi

Wasichana wengi hawapati elimu ya kutosha kuhusu afya ya uzazi na njia za kujikinga dhidi ya mimba zisizotarajiwa. Ukosefu wa maarifa haya huwafanya kuwa katika hatari ya kupata mimba za utotoni.

Charlotte (si jina halisi) mwenye miaka 16 mkazi wa Kijiji cha Kakese wilayani Mpanda, Mkoa wa Katavi ni mama wa mtoto mwenye miezi minne.

Anasema mabadiliko ikiwamo kuhisi usingizi kila wakati ndiyo yaliyomfanya mama yake kujua kuwa ni mjamzito.

Akiwa amesoma hadi darasa la sita anasema alipopata ujauzito baba wa mtoto alikataa mimba, lakini alipojifungua familia ya mwanamume ilikubali mtoto wa kiume aliyezaliwa ni wa kwao.

Hata hivyo, hawakuwahi kupeleka kitu chochote na kulazimika kuendelea kuishi nyumbani kwa mama yake, ambaye pia ana watoto wengine wanne.

Nilije Shija, mama wa Charlotte, anasema analea mjukuu kutokana na mama yake kutojua chochote kuhusu malezi ya mtoto.

Msichana mwingine Zoey (si jina halisi) mwenye miaka 16 anayeishi jirani na Charlotte ni mjamzito ambaye aliyempa ujauzito amekana kuhusika.

Mama wa Zoey anasema mwanaye wa kiume ameoa binti mwenye miaka 18 ambaye kwa sasa tayari ana watoto wawili.

Mila na desturi zinazokubali, kuhimiza ndoa za utotoni ni sababu nyingine kubwa. Katika jamii nyingi, ndoa za utotoni zinaonekana kama njia ya kumsaidia msichana au familia kupata mahari.

Katika baadhi ya vijiji wilayani Ileje, mwananchi imebaini uwepo wa dhana kwamba msichana kuanzia miaka 20 akiwa hayupo ndani ya ndoa hufanyiwa tambiko ikidhaniwa kwamba ana mkosi.

Kutokana na hilo, imekuwa kawaida kwa binti wa kuanzia miaka 15 kuolewa, ingawa hilo hufanyika kwa siri.

“Akifeli shule ni bora aolewe, asije kuzalia nyumbani akatupa aibu wazazi kuwa hatukumlea vyema,” anasema mmoja wa wazazi akisindikiza kauli yake na tabasamu.

Athari za mimba za utotoni

Kwa upande wa afya, wasichana wajawazito wenye umri mdogo wako katika hatari kubwa ya kupata matatizo ya kiafya, kama vile ugonjwa wa fistula, kifafa cha mimba, na vifo vya uzazi. Miili yao haijakomaa vya kutosha kushughulikia mimba na kujifungua.

Kwa mujibu wa Dk Medard Ndayanse, mimba ya chini ya miaka 18 mwanamke hajakomaa kiakili wala via vya uzazi, jambo ambalo huweza kumpa matatizo wakati wa ujauzito, kujifungua na baadaye.

“Hawa wapo katika hatari ya kupata kifafa cha mimba, kujifungua kabla ya wakati tofauti na kawaida mtoto anapokuwa tumboni anakomaa kwa kipindi cha wiki 37 hadi 40 sasa anapojifungua kabla ya wakati mtoto anakuwa hajakomaa,” anasema Dk Medard.

Anasema mabinti hao pia wapo katika hatari ya kupata watoto wenye uzito mdogo ikilinganishwa na uzito wa kawaida wa kilo 2.5 hadi 3.9.

“Sasa hawa wanakuwa katika hatari ya kupata watoto walio na uzito mdogo, hivyo huhitaji uangalizi maalumu ndiyo maana hulazwa kwani hali ya kutokomaa huwaweka katika urahisi kupata maambukizi,” anasema Dk Medard.

Anasema nyonga zao hazijakomaa jambo ambalo hufanya kushindwa kutanuka vizuri kuruhusu mtoto apite. Hali hiyo huweza kuchochea kujifungua kwa upasuaji na asipopasuliwa akabaki na uchungu na mtoto akashindwa kupita inaweza kumfanya apate fistula.

“Hawajajiandaa kuwa wazazi, kiuchumi na kisaikolojia. Wengine hupata mimba zisizotarajiwa hiyo inawafanya kuwa katika hatari ya kupata msongo wa mawazo,” anasema.

Mwanasaikolojia, John Ambrose anasema wasichana wengi walio na umri mdogo wanakuwa katika hatari ya kupata sonona baada ya kujifungua.

“Mara zote wanahisi kelele kama wanaambiwa unatakiwa uwe umesoma, uwe shuleni, una hili, akiwaza majukumu anayotakiwa kufanya kama mama, wengine huwa wanafikia kipindi cha kupiga mtoto kwa sababu wanakuwa na msongo wa mawazo wengine wanafikia hatua ya kutupa mtoto chooni,” anasema John.

Anasema wengine hushikwa na wasiwasi kiasi cha kushindwa kuwashika hata watoto wao.

Mimba za utotoni mara nyingi husababisha wasichana kuacha shule, hivyo kupunguza nafasi zao za kupata elimu na ajira nzuri baadaye maishani.

Hata hivyo, hivi sasa Serikali imetoa nafasi kwa wasichana hao kuendelea na masomo baada ya kujifungua.

Mimba inatajwa kuwa moja ya sababu inayofanya wasichana wengi kutoka katika mfumo rasmi wa elimu ambapo mwaka 2019, wasichana 1,135 wa shule ya msingi walipata ujauzito shuleni idadi ambayo ilishuka hadi kufikia 989 mwaka 2020.

Mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Aurea Simtowe (kushoto) akizungumza na Charllote (16) ambaye amebeba mtoto alipowatembelea nyumbani kwao katika Kijiji cha Kasese, wilayani Mpanda. Picha na Mpigapicha Wetu

Kwa upande wa sekondari katika kipindi hicho idadi ilishuka kutoka 5,398 hadi 4,543 mwaka 2020 kwa mujibu wa ripoti za Elimu za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), iliyotolewa Aprili 2022 ilibainisha wasichana 49,958 walipata mimba katika mwaka wa fedha 2021/2022, huku 20,698 wakiwa chini ya miaka 18.

Mtafiti wa Elimu, Muhanyi Nkoronko anasema ni vyema kudhibiti mimba za utotoni ili kuondoa pengo la elimu linaloweza kutengenezwa kati ya vijana wa kiume na kike waliopata elimu, jamii ione thamani hiyo badala ya kuwa chanzo.

“Hali hii isipodhibitiwa itaendelea kuongeza mzigo kwa Serikali, itaongeza idadi ya watu ambao itapaswa kuwagharamia katika huduma mbalimbali za kijamii na kuongeza utegemezi,” anasema Nkoronko.

Mimba za utotoni pia husababisha msichana na mtoto wake kuishi katika hali duni ya kiuchumi na kijamii, na hata unyanyapaa na kutengwa na jamii.

Nilije Shija mama wa Charlotte anasema, “kuanzia kujifungua, nililipa Sh400,000 ili afanyiwe upasuaji, upande wa mwanaume haukushiriki kwa chochote, ilifika wakati tukaanza kupelekana ofisi ya Serikali ya Kijiji ili wasaidie katika matunzo lakini bado hakuna mwangaza.”

“Nawaza mtoto akichangamka nimpeleke akajifunze kusoma cherehani, fedha zenyewe ndiyo hizi hadi ufanye vibarua huku na kule, ujikusanye,” anasema Nilije.

Diwani wa Kakese, Maganga Salaganda anasema tatizo la mimba limeendelea kupungua kutokana na vijana kuanza kujitambua na kutambua madhara ya mimba za utotoni.

Hata hivyo, anasema zinaongeza mzigo katika jamii, kwani wengi hukimbiwa na kuachiwa mzigo wa malezi.

Mtaalamu wa uchumi, Oscar Mkude anasema mara nyingi wasichana huathirika kwa kukosa fursa ya kuandaa maisha ya baadaye.

Anasema mimba za utotoni hupunguza nguvu kazi ya watu wanaoweza kuchangia katika pato la Taifa kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha.

Nkoronko anashauri kutolewa elimu ya jinsia na jinsi ili wasichana waweze kujua namna ya kujikinga na mimba za utotoni na umuhimu wa elimu.

Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wakawake Tanzania (Tamwa), Dk Rose Reuben anashauri kuwekwa kwa mifumo mizuri inayoimarisha taasisi ya familia.

“Mwaka 0 hadi 8 ni wakati ambao mtoto anatakiwa kuwa na malezi ya karibu na wazazi kwani kile anachofundishwa na kuaminishwa kinaweza kumsaidia katika maamuzi yake ya baadaye ya maisha yake,” anasema.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo katika ziara ndani ya mkoa huo amekuwa akiagiza wale wote wanaohusika kuwapa mimba wanafunzi kushughulikiwa.

Akiwa ziarani wilayani Momba alimuagiza Mkuu wa wilaya hiyo, Kenani Kihongosi kuwatafuta na kuwachukulia hatua wale wote waliosababisha mimba kwa watoto 194 walio chini ya miaka 18.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindiki amesema wanaendelea kushughulikia mila na desturi kuhakikisha haziendelei kuwa kichocheo cha mimba hizo.

Anasema ongezeko la mashirika yasiyo ya kiserikali katika mapambano ya mimba za utotoni limesaidia kuzipunguza.

Shirika la Plan International ni miongoni mwa yanayoshiriki katika mapambano ya kutokomeza mimba za utotoni mkoani Katavi kupitia mradi wa ‘Vijana na ubora malengo na afya (Vuma) unaotekelezwa kwa kushirikiana na Serikali, Umati na Taasisi ya Hope Center Tanzania.

Shirika hili huwafikia waliopo shuleni na walio nje ya mfumo wa shule, kupitia mitalaa iliyoandaliwa kukabili suala hilo.

Adella Ngusa, mtaalamu wa masuala ya jinsia anasema changamoto inayowakabili katika utekelezaji wa mradi ni mila na desturi za wafugaji na wakulima ambao wanaamini ng’ombe nyingi ni utajiri, hivyo  watu wenye hali ya chini wanapoletewa ng’ombe kama mahari huwa ngumu kukataa kumuozesha binti yao.

“Yuko tayari kumtoa binti yake hata kama yuko chini ya miaka 18 ili tu apate wale ng’ombe na hata kumkatisha masomo, pia jamii ya huku ni wakulima, kuna vipindi ambavyo wanahamia mashambani, hivyo tunashindwa kuwapata,” anasema Ngusa.

Anasema lengo la mradi huo wa miaka saba ulioanza mwaka 2022 hadi 2029 ni kupunguza mimba za utotoni kwa vijana na kuwapatia elimu za ujasiriamali hasa wanaoacha shule.

Imeandaliwa kwa msaada wa Bill & Melinda Gates

Related Posts