Pwani. Wafadhili kutoka Canada, wametoa Sh38 bilioni kusaidia shughuli za kilimo nchini kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Makali ya mabadiliko ya tabianchi yameendelea kuumiza vichwa vya mataifa tajiri duniani yanayotafuta suluhu na kuwezesha nchi zinazoendelea katika kupambana na hali hiyo.
Hata hivyo, mabadiliko ya tabia nchi yanagusa nchi zote na kwa Tanzania katika kilimo ambayo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa watu wengi.
Fedha zilizotolewa na Canada zinapitia Shirika la Care International la Tanzania na mradi wake utakuwa wa miaka sita katika wilaya za Iringa, Kilolo Mufindi, Wangi’ombe na Mbarali.
Katika mradi huo itatolewa elimu ya kilimo bora cha kisasa kinachozingatia utunzaji wa mazingira na itakuwa faida kwa mkulima moja kwa moja na mazingira hapa nchini.
Akizungumza baada ya kupokea ugeni wa Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada, Christina John ambaye ni Meneja Mwandamizi wa Rasilimali na Uhusiano wa Shirika la Care Tanzania amesema lengo ni kuongeza uzalishaji kwa mkulima na kutunza mazingira.
“Mradi huu utawanufaisha wakulima 175,282 moja kwa moja na watu zaidi ya 408, 992 kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika wilaya hizo. Faida nyingine wakulima watalima kilimo bora watatunza mazingira na watanufaika, pia hata mto Ruaha ambao upo katika ukanda huo utanusurika,” amesema.
Christina amefafanua kuwa katika mradi huo wakulima wataunganishwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) ili kufanya uamuzi wenye ushauri kutoka kwao.
Kadhalika mradi unalenga kusogeza huduma za ugani, teknolojia za kilimo, uwepo wa shamba darasa, kuwaunganisha na watoa huduma za pembejeo na kutunza vyanzo vya maji.
“Pia, mradi huu utaongeza mnyororo wa thamani kuanzia shambani hadi sokoni, pamoja na kuanzisha biashara zinazounga mkono mazao watakayoyazalisha,” amesema.
Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde ambaye alihudhuria uzinduzi wa mradi huo, amesema Serikali ya Tanzania imepokea msaada huo na unatarajia kuwanufaisha wanawake na vijana.
“Wanufaika wataweza kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa kuongeza uelewa, sisi jukumu letu tutaendelea kufuatilia na kuhimiza utunzaji wa mazingira,” amesema Silinde.
Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada, Ahmed Hussen amesema Canada ipo tayari kufadhili juhudi za utunzaji mazingira ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
“Mradi huu utanufaisha mazingira pamoja na mkulima, utawainua kutoka kwenye umasikini. Hii ni faida lazima tutunze mazingira yetu kwa faida na leo na kesho,” amesema.