Lindi. Vijana zaidi ya 50 wamepatiwa mafunzo ya utengenezaji wa vihenge ili kukabiliana na sumu kuvu.
Mafunzo hayo yametolewa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido)Mkoa wa Lindi.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi Mei18,2024 wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mratibu wa Kuendeleza Teknolojia, Mhandisi Abraham Malay amesema mafunzo hayo yamelenga kuwasaidia vijana kukabiliana na sumu kuvu kwa kuwapatia ujuzi wa utengenezaji wa vihenge vitakavyotumika kuhifadhia nafaka.
Malay amezitaja wilaya zilizoathiriwa na sumu kuvu kuwa ni Namtumbo mkoani Ruvuma, Nanyumbu na Newala mkoani Mtwara.
“Lengo la kuwapa mafunzo haya ni kwenda kutengeneza vihenge vitakavyohifadhiwa nafaka ambazo awali zilikiwa zinahifadhiwa kienyeji,” amesema Malay.
Meneja wa Sido Lindi, Frida Mhunguru amewataka vijana hao kwenda kutumia elimu waliyoipata kuwafundisha wengine ili kukabiliana na sumu kuvu.
“Mmepata mafunzo pamoja na ujuzi,mwende mkautumie vizuri ujuzi huu, sio mkitoka hapa mnakwenda kukaa mtakuwa hamjafanya kitu,”amesema Mhunguru.
Akifunga mafunzo hayo, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Lindi, Stanford Mwakatage ameishukuru Serikali kwa kuwajengea uwezo vijana wa katika ufundi.
“Naipongeza Serikali kwa juhudi kubwa wanayofanya kwa kuwapa mafunzo vijana ili waweze kujiajiri pamoja na kuondokana na changomoto mbalimbali, niwaombe pia vijana mkafanye kazi na mkatumie vema ujuzi mliopewa,”amesema Dk Mwakatage.
Mwanafunzi Ayubu Mbaruk amesema ufundi walioupata utasaidia kuwajengea uwezo vijana wengine kwa kuwa watakuwa wanatoa elimu kwa wenzao.
“Mim ni mkazi wa Mtwara, lakini nimekuja kujifunza jinsi ya kutengeneza vihenge, naishukuru Serikali kwa kutuona sisi vijana na kupewa mafunzo, elimu hii niliyoipata nitakwenda kuwafundisha na wenzangu ambao hawakuweza kuja,”amesema Mbaruku.