Utata askofu aliyedaiwa kujinyonga | Mwananchi

Dodoma. Utata umeibuka kuhusu  kifo cha Askofu Mkuu wa Makanisa ya Methodist, Joseph Bundala, baada ya ndugu kusema hakujinyonga kama ilivyosemwa na Jeshi la Polisi, ikidai alikuwa akipokea vitisho kabla ya kifo chake.

Askofu huyo alikutwa amejinyonga ndani ya choo kwenye ofisi yake iliyopo katika kanisa hilo eneo la  Meriwa jijini Dodoma Mei 16, mwaka huu.

Msemaji wa familia hiyo, Tito Kasuga amesema leo kuwa wana wasiwasi juu ya kifo cha ndugu yao kutokana na mazingira ambayo waliyakuta katika eneo la tukio.

Amesema kwa kuwa Serikali ina mkono mrefu, wanaomba kufanyika uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini ukweli.

Kasuga amesema wamelazimika kutoa taarifa hiyo kutokana na mitandao ya kijamii kutoa taarifa kuwa ndugu yao alikutwa amejinyonga, jambo ambalo kwao halina ukweli.

“Kwa hiyo tunaiomba Serikali ilifanyie uchunguzi jambo hili ili kubaini chanzo na sababu kubwa ni kuwa alikuwa akipokea vitisho kupitia simu zake, kwa hiyo tuna mashaka ya tukio zima la kuondoka kwa mpendwa wetu katika mazingira haya,” amesema.

Amesema baada ya polisi kukamilisha uchunguzi wao, watamzika Jumatatu badala ya kesho kama ilivyokuwa imeamuliwa awali.

Dada wa marehemu, Veronica Alexandra amesema siri ya marehemu ni siri yake. Amesema Mei 16, mchana alimpigia simu akimweleza amepokea simu za vitisho.

“Ameniambia dada hapa naona akili yangu imefika mwisho, simu zinanitisha. Nikamwambia naomba ujipe moyo, lakini saa 10.00 jioni, nilianza kumtafuta sikumpata tena,” amesema.

Amesema jambo hilo lilimpa hofu na kwamba saa 2.00 usiku alipata taarifa za kifo chake.

“Mazingira tuliyoyakuta, hata wewe usingeamini kama yule ndugu amejinyonga. Ninaungana na mwanafamilia aliyetoa tamko kuwa Serikali itusaidie kufuatilia hili tukio kwa karibu zaidi kwa sababu ushahidi upo hadi kwenye simu,” amesema.

“Unapokuja kutuambia kuwa amejinyonga alikuwa anadaiwa, hata Serikali inadaiwa, hata mimi nadaiwa, vile vitisho hatujui vilitoka wapi, tunaamini kuwa ndugu yetu hajajinyonga,” amesema Veronica.

Juzi Mwenyekiti wa Mtaa wa Meriwa, Gervas Lugunyale alisema aliitwa na mmoja wa wachungaji wa kanisa hilo (ambaye hakumtaja jina) na alipokwenda walikuta kwenye meza iliyopo ofisini kwake (marehemu), kuna waraka ambao uliandikwa madeni anayodai na anayodaiwa.

Amesema kabla ya tukio hilo, mchungaji wa kanisa hilo (hakumtaja jina) alimweleza kuwa aligizwa na askofu huyo kwenda dukani kumnunulia biskuti na soda.

Amesema baada ya kununua vitu hivyo alikwenda kwenye kipindi Makole akamuacha askafu huyo pekee ofisini na alipore-jea saa 1.00 usiku alikuta mlango uko wazi na ndani kuna giza.

Baada ya kufuatilia ndipo alipoona waya wa simu umefungwa kwenye dirisha na mwili wake ukiwa hapo kwenye choo ndani ya ofisi yake.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Alchelaus Mutalemwa, amesema Jeshi hilo linachunguza tukio la kujinyonga kwa askofu huyo.

“Uchunguzi katika eneo la tukio umekutwa ujumbe unaeleza sababu za kujinyonga ni madeni na mgogoro uliopo katika uendeshaji wa shule binafsi. Uchunguzi bado unaendelea,” amesema Mutalemwa.

Related Posts