Dar es Salaam. Katika ufanyaji wa shughuli za kila siku mtu huweza kuumia kutakapomsababishia majeraha mbalimbali katika mwili.
Kwa mujibu wa tovuti ya Wikipedia, majeraha ni vidonda vitokanavyo na ajali ya ghafla ambayo husababisha ngozi kukatwa, kuchomwa au kudhurika kwa namna nyingine.
Inapotokea mtu amepata majeraha katika mwili hufanya jitihada mbalimbali zitakazomwezesha kupona kwa haraka, ikiwemo kupata huduma ya kwanza pamoja na kwenda hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.
Pamoja na kupatiwa matibabu, wataalamu wa afya wanaeleza kuwa na lishe bora ili kuwezesha mwili kupata virutubisho ambavyo kwa kiasi kikubwa inasaidia jeraha kupona kwa haraka.
Akizungumza na Mwananchi, Meneja mradi wa Afya ya Mama na Mtoto na mtaalamu wa lishe kutoka Shirika la Word Vision, Dk Daudi Gambo anasema ili mtu aliyepata majeraha aweze kupona kwa haraka anatakiwa kula zaidi vyakula vyenye wingi wa protini kama vile nyama, mayai, samaki na vile vya jamii ya maharage, kwani vitasaidia katika kujenga na kukuza tishu za mwili hivyo kusaidia jeraha kupona kwa haraka.
Anasema pamoja na protini anahitajika kula matunda pamoja na mboga za majani zitakazosaidia kuupa mwili vitamini, madini na virutubisho asili ambavyo ni muhimu kwa kujenga kinga imara ya mwili.
“Katika matunda na mboga za majani yanapatikana madini ya chuma ambayo yatamsaidia kuongeza damu mwilini ambayo pengine ilitoka alipopata jeraha, madini mengine muhimu kama vile zinki, potasiamu, kalsiamu, magneziamu, kwa ajili ya kuimarisha afya ya mwili wake.
“Vitamini kama vile A, B, C, D na E ambazo ni muhimu kuhakikisha kuwa ana kinga bora ya mwili wake.”
Kwa upande wake Dk Samweli Msigwa, anaongeza kuwa pamoja na vyakula, ni muhimu kuzingatia unywaji wa maji ya kutosha kama inavyoshauriwa na wataalamu angalau lita moja na nusu hadi tatu ili kuzuia upungufu wa maji na madini ambao unaweza kusababisha kukakamaa kwa misuli.
“Pia yanasaidia katika kuboresha kinga mwili, hivyo kuwezesha jeraha kupona kwa haraka,” anaongeza.
Vilevile anaongeza kuwa ili jeraha liweze kupona kwa haraka ni muhimu mhusika kujiepusha na ulaji wa vyakula vyenye sukari na mafuta mengi na vile vyenye wingi wa kafein.
“Pamoja na vyakula, vilevile ili majeraha yaweze kupona kwa haraka ni muhimu kuzingatia ushauri unaotolewa na daktari wakati wa kupatiwa matibabu pamoja na matumizi sahihi ya dawa kama ilivyoshauriwa pamoja na usafi wa mwili”