Wanafunzi wataka pedi ziondolewe kodi, zitolewe bure shuleni

Dar es Salaam. Katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Hedhi Salama Duniani Mei 28 mwaka huu, wasichana kutoka shule mbalimbali za msingi na sekondari nchini wametoa mapendekezo manne ikiwamo kuiomba Serikali kuondoa kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika taulo za kike (Sodo).

Pendekezo lingine ni ugawaji wa pedi bure kwa wasichana wote walioko shuleni ili kuwasaidia kusoma kwa uhuru na kupunguza utoro jambo litakalowezesha kuongeza ufaulu kwa wasichana.

Mapendekezo hayo yametolewa jana Ijumaa Mei 17 2024 katika uzinduzi wa Kampeni ya Wasichana ya Pedi Bure, Pedi Bila Kodi iliyoanzishwa na  mashirika ya Msichana Initiative na Pastoral Women Council (PWC) kwa lengo la  kuonesha umuhimu na uharaka kwa Serikali na wadau kutengeneza mazingira wezeshi ya kupata bidhaa za kujihifadhi wakati wa hedhi.

Kampeni hiyo inaongozwa na wasichana vinara 50 ambao wako ndani ya mfumo wa rasmi wa elimu na wasichana ambao wako nje ya mfumo wa elimu kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Dodoma, Arusha na Tabora.

Akizungumza kwa niaba ya wasichana wengine, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Emanyata iliyopo Arusha Elizabeth Mollel amesema kutokana na baadhi ya wasichana kushindwa kumudu gharama za kupata taulo za kike kila mwezi, huishia kutumia vifaa kama vile, vipande vya nguo, majani ya miti, na vifaa vingine ambavyo si salama kwa afya ya wasichana.

Elizabeth amesema pakiti moja ya taulo za kike inauzwa kwa Sh2,000 na inaweza kuwa juu zaidi kulingana na kampuni  na mahali.

Amesema msichana atahitaji kuanzia pakiti mbili na zaidi ili kukamilisha mzunguko wake wa hedhi wa mwezi mmoja.

“Ukiangalia gharama hii ni kubwa sana, hasa kwa wasichana wanaotoka katika kaya masikini ambazo taulo za kike sio kipaumbele katika bajeti ya familia.

“Ukosefu wa taulo za kike unachangia wasichana kujiingiza katika tabia hatarishi na kujiingiza katika mahusiano katika umri mdogo ili apate fedha zitakazomuwezesha kununua taulo hizo,”amesema Elizabeth.

Amesema sambamba na kutoa pedi bure na kuondoa kodi kwenye taulo za kike, bado kuna umuhimu wa kuwa na vyumba salama vya kujistiri wanapokuwa shuleni.

“Ukosefu wa mazingira salama ya kujihifadhi shuleni ni moja ya sababu inayochangia utoro wa wasichana kwa siku tatu hadi saba kila mwezi,” amesema.

Vilevile amewataka wadau wa haki za wasichana waendelee kutoa elimu kuhusu masuala ya hedhi salama na umuhimu wa elimu ili kuendelea kubadilisha maisha ya wasichana na jamii ya Kitanzania kwa jumla.

Mkurugenzi Mtendaji wa Msichana Initiative, Rebeca Gyumi amesema wao kama moja kati ya taasisi zinazotetea haki za wasichana, watahakikisha sauti za mabinti hao zinasikika ili mamlaka husika zione ni namna gani inazifanyia kazi.

“Kupitia kampeni hiyo, tutafanya mikutano mbalimbali ya kukutana na wanajamii, wasichana wenzetu, pamoja na wafanya maamuzi wakiwamo wabunge ili kuhakikisha tunafikia azma yetu ya pedi bure, pedi bila kodi,” amesema Gyumi.

Ofisa Miradi kutoka PWC, Nang’ambo Mollel amesema pamoja na jitihada zinazofanyika bado kuna kazi kubwa ya kuielimisha jamii kuondokana na imani potofu.

“Sisi wasichana vinara tunaamini hedhi ni tunu na hedhi ni mwanzo wa maisha ya mwanadamu, hivyo ni suala ambalo linapaswa kupewa kipaumbele kwa ustawi wa wasichana na Taifa letu kwa jumla,” amesema Mollel.

Related Posts