Arusha 18 Mei 2024 – Wanahisa wa Benki ya CRDB wameidhinisha kwa kauli moja mapendekezo ya Bodi ya Wakurugenzi kuhusu malipo ya gawio la Shilingi 50 kwa kila hisa jambo linalofanya jumla ya thamani ya gawio la mwaka wa fedha 2023 kufikia Shilingi bilioni 130.6, sawa na 30.9% ya faida halisi.
Katika taarifa yake wakati wa Mkutano Mkuu wa 29 wa Benki hiyo uliofanyika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Mwenyekiti wa Bodi ya Benki hiyo Dkt. Ally Laay alisema gawio lililoidhinishwa kwa kila hisa ni ongezeko la asilimia 11 ikilinganishwa na Shilingi 45 kwa kila hisa iliyotolewa jana, ikiashiria ukuaji mkubwa wa mapato kwa kila hisa kufikia Shilingi 161.9 ikilinganishwa na Shilingi 134.1 mwaka 2022.
“Kwa mara nyingine tena, tunafuraha kuwatoa thamani endelevu kwa wanahisa wetu. Utendaji wa Benki mwaka 2023 ulikuwa mzuri, ikiwa ni uthibitisho wa mafanikio ya mkakati wetu mpya wa miaka mitano wa muda wa kati wa 2023 – 2027. Benki yetu na kampuni zake tanzu ilipata faida halisi ya Shilingi 422.8 bilioni, ongezeko la 20.3%,” alisema Dkt. Laay.
Alibainisha zaidi kuwa kampuni tanzu za Benki ya CRDB zilitoa mchango chanya kwa mwaka uliopita. CRDB Bank Burundi ilipata ukuaji mzuri wa 30.7% katika Faida Baada ya Kodi, na kufikia Shilingi 30.2 bilioni. Amesema pamoja na kampuni za CRDB Bank Congo na CRDB Insurance Company Ltd kutotengeneza faida, kampuni hizo zimeonyesha mwanzo mzuri unaoashiria kuwa na mchango mkubwa katika siku za usoni. Jumla ya mchango wa kampuni tanzu kwenye Faida Baada ya Kodi ulikuwa 6%.
“Ninafurahia kuona juhudi zetu za upanuzi za kikanda zinaleta matokeo chanya. CRDB Bank Burundi imefanikiwa kuongoza kwa faida katika soko la nchi hiyo katika kipindi cha robo ya kwanza ya 2024. Zaidi ya hayo, kampuni yetu ya nchini DRC imepokelewa vizuri nchini humo tangu kuanzishwa kwake mwezi Julai 2023, na kuvutia wateja na biashara nyingi nchini humo,” aliongeza.
Afisa Mkuu wa Fedha, Fredrick Nshekanabo, aliripoti kuwa Mizania ya Benki ya CRDB na kampuni zake tanzu imeendelea kuimarika ikishuhudia ukuaji wa mwaka wa 14.5% kutoka shilingi trilioni 11.6 mwaka 2022 mpaka shilingi trilioni 13.3 mwaka 2023. Ukuaji huo ulichangiwa zaidi na ongezeko la 22.8% la mikopo kufika shilingi trilioni 8.4 ikichangiwa na ongezeko la amana za wateja zilizopanda kwa 8.0%, mikopo kwa 73.9%, na kukua kwa mtaji wa wanahisa kwa 20.4%.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesisitiza kuwa mkakati mpya wa biashara umekuwa muhimu kwa mafanikio ya benki, ukifanya kazi kama ramani ya kuboresha utendaji kazi. Amesema kwa sehemu kubwa Benki ya CRDB ilijikita katika uwekezaji kwenye mifumo ya kidijitali, huku akieleza kuwa benki imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa mradi wa mfumo mkuu mpya wa uendeshaji wa benki (CBS).
Nsekela pia alisema kuwa Benki ya CRDB imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kukuza ujumuishi wa kifedha, kwa wajasiriamali na wafanyabiashara. Kupitia mpango wa IMBEJU taasisi ya CRDB Bank Foundation imeboresha uwezeshaji kwa vijana na wanawake. Zaidi ya hayo, Benki imeunda ushirikiano wa kimkakati ili kufadhili vyema miradi ya maendeleo nchini.
Nsekela alielezea mipango ya siku za usoni ya Benki ya CRDB na kampuni zake, akisisitiza kuongeza kwa mchango wa kampuni tanzu zilizoanzishwa, kuboresha huduma kwa wateja na kuwekeza zaidi katika ubunifu wa kidijitali. Kadhalika, amesema Benki hiyo itaendelea kuongeza usimamizi mkubwa katika vihatarishi, na kuhakikisha inaendana na mabadiliko ya usimamizi, na kuhakikisha utawala bora.
Kwa upande mwingine, Wanahisa wa Benki ya CRDB waliidhinisha kampuni ya Price Water Coopers (PWC) kama Wakaguzi wa Nje wa Benki kwa mwaka wa fedha wa 2024. Wanahisa wa Benki pia walichagua tena Wajumbe wawili wa Bodi, Prof. Faustine Bee kuwakilisha wanahisa wenye umiliki chini ya 1%, na Gerald Kassato kuwakilisha wanahisa wenye hisa kati ya 1% na 10%.
Akizungumzia malipo ya gawio hilo, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo na Mbunge wa Vunjo, Dkt. Charles Kimei, alieleza kufurahishwa kwa wanahisa kwa kuendelea kupata ongezeko la gawio, akibainisha kuwa hisa za benki hiyo zimebakia kuwa chachu ya wawekezaji kwasababu benki haijawahi kushindwa kulipa gawio kwa wanahisa wake.