Kibaha. Kambi ya Ruvu JKT Kibaha Mkoa wa Pwani imeanza kuingiza aina mbalimbali za wanyama kutoka porini ndani ya eneo lenye ukubwa wa zaidi ya eka 70.
Kikosi hicho cha jeshi, kimetenga eneo hilo kwa lengo la kuanzisha bustani ya wanyama ambao baada ya kuwatoa porini wanawapa mafunzo ya namna ya kuishi na binadamu ili kutowapa madhara watu pindi wanapofika kufanya utalii.
Katika utekelezaji wa mkakati huo, mpaka sasa uongozi wa kikosi hicho umeshafikisha aina nane za wanyama ndani ya bustani hiyo ambao ni twiga,nyumbu,pundamilia,pofu,swala,paa,pongo na mbuni.
Akizungumza leo Jumamosi Mei 18,2024 wakati wa uzinduzi wa bustani hiyo, Kamanda wa Kikosi cha Ruvu (JKT ) Kanali Peter Mnyani amesema hiyo ni hatua ya awali kwa kuwa malengo yaliyopo ni kuongeza wanyama wa aina mbalimbali akiwamo simba ifikapo Juni mwaka huu.
Kanali Mnyani amesema lengo la kuanzisha bustani hiyo ni kukuza uchumi na kuendelea kuongeza maarifa kwa vijana wanaofika kupata mafunzo ya kijeshi ndani ya kambi hiyo pamoja na kuwa na kivuto cha utalii.
“Kama unavyoona hawa ni wanyama wa porini lakini wamekuwa rafiki wa binadamu mtu anamkaribia anamshika twiga na mbogo na kupiga nao picha na hii inatokana na mafunzo wanayopewa mara tunapowachukua kutoka mapori mengine,”amesema Kanali Mnyani.
Ameeleza namna kikosi hicho kitakavyonufaika na uwepo wa bustani hiyo kuwa ni kuongeza pato litakalotumika kuhudumia vijana wanaopita kwenye kambi hiyo kupata mafunzo.
Wakizungumza baada ya uzinduzi wa bustani hiyo baadhi ya wakazi Mkoani humo wamesema uwepo wa eneo hilo utawapunguzia gharama ambazo wamekuwa wakizitumia kulipa nauli kwenda mikoa ya mbalimbali kujionea wanyama.
“Tumekuwa tukisafiri umbali mrefu kwenda kufanya utalii na wakati mwingine kwenye bustani za wanyama zinazomilikiwa na watu binafsi, lakini leo tumeletewa mlangoni na Serikali ni jambo la kushukuru,”amesema Zainabu Issa.
Naye Hassani Abedi amesema ubunifu uliofanywa na kikosi hicho kwa kuanzisha bustani ya wanyama unapaswa kuigwa na vikosi vingine nchini kwa kuwa mbali na kujiongezea kipato, pia utawezesha jamii kujenga uhusiano bora na majeshi hususa pale wanapofika kufanya utalii wa ndani.
Awali, mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon amewataka wakazi wa mkoa huo kujiwekea utaratibu wa kutembelea bustani hiyo kwa kuwa kwa kufanya hivyo watakuwa wanachangia uchumi wa nchi.
Amesema ubunifu uliofanywa na kikosi hicho si tu kuwa una faida ya kuongeza uchumi pekee bali unalenga hata kulinda mazingira ambayo Serikali imekuwa ikisisitiza taasisi na wananchi kuzingatia hilo.