Na Mwandishi wetu, Arusha
KAMPUNI ya Barrick nchini, imedhamini na kushiriki katika kongamano la wanafunzi wa vyuo vikuu lililoandaliwa na taasisi ya kuchipua na kuendeleza vipaji vya uongozi kwa vijana (AIESEC Tanzania) lililofanyika katika Chuo cha Uhasibu cha Arusha na kuwashirikisha wanafunzi, wahadhiri na wadau mbalimbali.
Kupitia kongamano hilo ambalo hufanyika kila mwaka, wanafunzi huweza kufahamu jinsi taasisi mbalimbali nchini zinavyoendesha shughuli zake lengo kubwa likiwa ni kuwajengea uwezo wa kujua vipaji walivyonavyo, kujifunza jinsi ya kujiamini na kukabiliana na ushindani katika soko la ajira, kujitambua uwezo wao ni jinsi gani wanaweza kushiriki kutoa mchango wa kuendeleza taifa pindi wamalizapo masomo yao.
Maofisa Rasilimali Watu Waandamizi wa Barrick pia walishiriki katika maonesho na kongamano hilo ambapo walipata fursa ya kuzungumza na wanafunzi kuhusiana na kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ajira,kuendeleza vipaji vyao pia wanafunzi walipata fursa kuelewa jinsi kampuni ya kimataifa ya Barrick, inavyoendesha shuguli zake kwa kutoa kipaumbele kusaidia jamii sambamba na mpango wake wa kuibua na ukuzaji wa vipaji kwa vijana wa kitanzania na wafanyakazi wake.
Mwisho