YANGA nzima jana ilikuwa Arusha ikitafuta tiketi ya kucheza fainali ya tano ya Kombe la Shirikisho (FA) ndani ya miaka tisa, lakini mabosi wake wakirudi tu mjini, watakutana na bilionea mmoja Mkongomani anawasubiri kwa jambo moja tu zito la usajili wa beki wao mpya.
Bilionea Jacques Kyabula Katwe yuko nchini tangu jana na alitua na ndege binafsi akitokea nchi moja ya Afrika, lakini hapa anataka kuonana na mabosi wa Yanga kumalizia mazungumzo ya usajili wa beki wake, Chadrack Boka anayetakiwa na mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara mara 30.
Mmoja wa wasaidizi wa Katwe aliliambia Mwanaspoti Katwe atakutana na mabosi wa Yanga leo Jumatatu kumalizia usajili wa beki huyo, baada ya awali vigogo hao kukutana jijini Lubumbashi, DR Congo wakati Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said alipokwenda kumtazama beki huyo wa kazi.
Katwe ndiye Gavana wa Jiji la Hauti-Katanga, DR Congo na ni Mwenyekiti wa FC Lupopo yenye upinzani mkubwa na TP Mazembe kwenye ligi kuu ya DR Congo na jamaa anaendelea kuijenga timu hiyo kuwa tishio nchini humo.
Lupopo ambayo anaitumikia mshambuliaji wa zamani wa Geita Gold, George Mpole, bila fedha ya Katwe ni sawa na hakuna kitu kwani tajiri huyo anaipa nguvu kubwa ya kifedha kwa kusajili mastaa wa maana.
Mbali na vikao vyake na Hersi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Klabu Afrika (ACA) pia Katwe huenda akakutana na tajiri wa Yanga, Ghalib Said Mohammed (GSM) ambaye wanafahamiana kibiashara wakiwahi kukutana jijini Lubumbashi wakati Yanga ilipokwenda kuichapa TP Mazembe kwenye mechi za Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi msimu uliopita.
“Atamsubiri Rais wa Yanga, bahati mbaya amekuta ameshaondoka lakini kwa heshima atamsubiri. Unajua bosi Katwe ni mtu asiyependa kuonekana yuko juu, amepitia hapa Tanzania kutokana tu na heshima ambayo Rais wa Yanga aliwapa Lupopo ili wamalizie hatua ya usajili wa Boka,” alisema msaidizi huyo wa Katwe.
“Nadhani atakutana pia na GSM kwani wanafahamiana sana. Wakati Yanga ilipokuja Congo kucheza na Mazembe waliwahi kukutana, kama GSM yupo nchini watakutana pia.”
Yanga inataka kumsajili Boka kutoka Lupopo kuja kuziba nafasi ya mkongwe Lomalisa Mutambala ambaye ataachana na timu hiyo mara baada ya mkataba wake kumalizika mwisho wa msimu huu.