Chuo Kikuu Kampala chakubali yaishe, kuilipa NSSF Sh4 bilioni

Dar es Salaam. Wamemalizana. Ndiyo neno unaloweza kulitumia kuelezea uamuzi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa Kampala nchini Tanzania (KIUT) kuomba kumalizana na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) nje ya Mahakama na kuulipa Sh4 bilioni.

Hii ni baada ya Bodi ya Wadhamini ya NSSF kufungua kesi ya madai namba 2 ya mwaka 2023 dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya KIUT, ikiomba Mahakama iiamuru KIUT kulipa fedha hizo ambazo ni malimbikizo ya michango ya wafanyakazi wake.

Fedha hizo ni malimbikizo ya michango wa wafanyakazi wa KIUT ambao ni wanachama wa NSSF kwa kipindi cha kati ya Novemba 2018 hadi Novemba 2023.

Agosti 14, 2023, Mahakama Kuu ya Tanzania masjala ya Dar es Salaam iliipa KIUT kibali cha kufika mbele yake kujitetea na kuwasilisha majibu ya madai dhidi yake kwa maandishi, amri ambayo ilitekelezwa kwa wakati na wadaiwa.

Katika kujibu madai hayo, KIUT kwenye maelezo yake ya Agosti 31, 2023, iliiomba Mahakama iyatupe maombi ya NSSF ikidai hayana mashiko.

Hata hivyo, wakati shauri likiendelea katika hatua mbalimbali, KIUT ilionyesha nia ya kumalizana na NSSF nje ya Mahakama na kuuandikia barua mfuko huo, kujifunga kuwa italipa fedha hizo kwa awamu 20; yaani Sh200 milioni kila mwezi.

Hukumu ya Jaji Dyansobera

Baada ya hatua hiyo, Jaji Wilfred Dyansobera katika hukumu yake ya Mei 17, 2024, amesema pande zote mbili zimeridhia kulimaliza suala nje ya Mahakama.

Amesema zimekubaliana wadaiwa katika shauri hilo kuilipa NSSF fedha zote – Sh4.015 bilioni wanazodaiwa.

Kulingana na makubaliano hayo ambayo wameyasajili mahakamani kama hukumu rasmi, KIUT itakuwa inailipa NSSF Sh200 milioni kila mwezi ambazo ni malimbikizo ya michango ya wanachama wake.

Baada ya kutimiza masharti hayo, Jaji Dyansobera alisema kutakuwa hakuna haki zaidi baina ya pande hizo mbili mara baada ya kusainiana makubaliano hayo.

Related Posts