Ihefu yafunguka ishu ya Banda

UONGOZI wa Ihefu umeweka wazi kushtushwa na taarifa zinazosambaa zikimhusu aliyekuwa nyota wa zamani wa Simba, Mmalawi, Peter Banda za kudai kusainishwa mkataba na timu hiyo kisha kutolipwa fedha za usajili.

Banda aliyewahi kuichezea Simba kwa misimu miwili kuanzia mwaka 2021 hadi 2023 kisha kurudi Nyassa Big Bullets ya kwao Malawi, alidai alisainishwa na Ihefu mkataba kipindi cha dirisha dogo msimu huu ingawa hakulipwa pesa zake za usajili.

Nyota huyo wakati anazungumza na gazeti la National la Malawi alisema, aliletewa mkataba na tiketi ya ndege ya kuja hapa Tanzania ila hawakumwingizia chochote kwani amekaa muda mrefu na hakusaini timu nyingine kwa sababu alikuwa na mkataba nao.

Baada ya madai hayo, Mwanaspoti lilimtafuta Mtendaji Mkuu wa Ihefu, Olebile Sikwane aliyeweka wazi hata yeye ameshtushwa na taarifa za nyota huyo, kwani hawakuwahi kumsajili na wachezaji wote waliowasajili wako nao kikosini mwao.

“Ndugu yangu kwa sasa niko Saudi Arabia, lakini kuhusu hizo taarifa nimeziona na zimenisikitisha kwa kweli, kutokana na majukumu tuliyokuwa nayo kwa sasa muda ukifika tutaweka wazi juu ya hilo ila nikuhakikishie hatujamsajili,” alisema.

Kwa upande wa Ofisa Habari wa Ihefu, Peter Andrew alisema hata yeye ameona taarifa hizo ingawa kwa sasa wao kama klabu wamewekeza nguvu zao kwenye mchezo wa nusu fainali dhidi ya Yanga uliochezwa jana na baada ya kumaliza watafafanua ikiwa wanaona inafaa.

“Mchezaji kushika mkataba wa timu fulani haina maana ndio ameusaini, unaweza ukawa unamhitaji mchezaji kweli ila mwishoni ukamkosa na hilo ni jambo la kawaida tu kutokea, wachezaji tuliowasajili msimu huu ndio hawa tuliokuwa nao.”

Msimu huu nyota huyo alihusishwa kurudi Tanzania kujiunga na Ihefu ama KMC ambazo zote hazikuweza kumsajili.

Related Posts