MCHEZAJI kinda wa Kitanzania, Jabir Seif Mpanda anayenolewa Hispania katika akademi ya Getafe, amechekelea rekodi aliyoweka Jumatano ya wiki iliyopita huko Saudi Arabia wakati timu ya taifa ‘Taifa Stars’ ikicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Sudan.
Katika mchezo huo wa kirafiki ambao Stars ilipoteza kwa mabao 2-1, Jabir aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi, miaka 17 na siku 98 kuichezea timu hiyo ya Taifa la Tanzania ambayo kwa sasa ipo chini ya kaimu kocha mkuu, Hemed Suleman ‘Morocco’.
Mara baada ya mchezo huo, Jabir ambaye safari yake ya soka ilianzia nyumbani Tanzania kabla ya kwenda Uingereza, alieleza furaha yake kwa kusema anatoa shukrani zake kwa kocha wa Stars (Morocco) na Shirikisho la soka nchini (TFF) na wadau kwa imani ambayo wameonyesha juu yake.
“Kiukweli hii ilikuwa ndoto yangu tangu nikiwa Uingereza katika akademi ya Buckswood, niliamini kuna siku nitapata nafasi ya kuichezea Taifa Stars. Nilikuwa nikiwaambia vijana wenzangu na hata familia yangu kwa sababu imekuwa ikinisapoti kwa kila hatua,” anasema na kuongeza;
“Hatimaye kile nilichokuwa nikikiota kimetimia tena nikiwa na umri mdogo, nashindwa kueleza vizuri lakini hii ni hamasa tosha na heshima kubwa kwangu na hata familia yangu, kilichopo ni kuendelea kuamini katika ndogo na kuendelea kujituma.”
Jabir aliweka rekodi hiyo dakika ya 78 akichukua nafasi ya Ben Starke anayecheza soka la kulipwa Uingereza akiwa na klabu ya Likestone Town na ndani ya dakika 12 alizocheza aligusa mpira mara 14 huku akitumika kama winga nafasi ambayo pia amekuwa akiimudu.
Akizungumzia kiwango cha mchezaji huyo, Morocco alisema amefurahishwa na mwenendo wa wachezaji wote vijana waliocheza mchezo huo huku akiweka wazi ni maandalizi kwa ajili ya mashindano ya Mataifa ya Afrika (Afcon).
“Kwanza mimi ni muumini sana wa wachezaji vijana na niko tayari kuwasapoti ili kutengeneza kizazi kizuri kijacho, mwaka 2027 tutakuwa wenyeji wa Afcon, hivyo ni muda mwafaka wa kuwaandaa ili waendelee kupata uzoefu wa mashindano mbalimbali.”
Morocco aliongeza, licha ya kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Sudan, ila hakuangalia zaidi matokeo isipokuwa aliangalia namna bora ya kuwajenga wachezaji vijana ili kuwaunganisha na wakubwa jambo ambalo ameona lina mwangaza huko mbeleni.
Jabir alitua Hispania mwaka 2021 na anacheza soka la kulipwa kwa sasa akitokea Uingereza katika akademi ya Buckswood.
Mbali na uhamisho huo kujikita kisoka kulingana na fursa mbalimbali ambazo zilionekana pia alikuwa akiendelezwa kielimu. Maisha yake ya soka Hispania yalianzia jijini Valencia alikojiunga na akademi ya SPF na alidumu hapo kwa kipindi kifupi ndipo alipopata nafasi ya kufanya majaribio na kufuzu Getafe.
Rekodi ambayo Jabir ameiweka imemwibua kocha wake huko Getafe, Alvaro Fernandez na kusema, “Hakuna asiyejua ni mchezaji mwenye juhudi na nidhamu kubwa ya kujifunza, kuwa na kipaji peke yake haitoshi.”
“Ametuheshimisha lakini anatakiwa kuendelea kukua katika mwelekeo mzuri ili kuwa mmoja wa wachezaji watakaokuwa msaada kwa taifa lake, binafsi namwona mbali, kikubwa ni kumwamini na kumpa nafasi bila kuchoka, sio kila mchezaji anaweza kukupa matokeo ya papo kwa hapo.”
Jabir ni mtoto wa kwanza katika familia ya Seif Mpanda, ana wadogo zake wawili ambao wapo Hispania, mmoja ni Tariq na mwingine Barka na wote wapo katika vituo vya kulea vipaji kwa ajili ya kuendelezwa.
Kinda huyo anayependa kushambulia akitokea pembeni akiwa Hispania amekuwa akivutiwa kwa karibu kiuchezaji na Vini Jr ambaye amekuwa moto wa kuotea mbali akiwa na Real Madrid na timu yake ya taifa la Brazil.
KWANINI VINI JR
Anasema ni kutokana na utofauti ambao yupo nao, amekuwa akicheza kitimu zaidi tofauti na mawinga wengine,”Wapo wachezaji wazuri ambao ukisema uwaorodheshe orodha itakuwa ndefu sana, lakini binafsi huwa navutiwa na mchezaji ambaye anacheza kwa ajili ya kusaidia timu,”
“Wapo mawinga ambao hucheza kwa ajili ya kuonekana na sio maslahi ya timu, Vini Jr ni tofauti sana ndio maana nimekuwa nikimfuatilia na kwa bahati nzuri niliwahi kupata nafasi ya kumtazama Santiago Bernabeu.”
“Sitaki kuwa yeye, nataka kuwa mimi lakini ni vizuri kujifunza kutoka kwa wachezaji ambao wanafanya vizuri,”anasema kinda huyo.
WADAU WAFUNGUKA
Nyota wa Kettering Town, Adi Yussuf ambaye pia amekuwa akiwanoa vijana wa Leicester City, amefurahishwa na mpango wa Taifa Stars kutoa nafasi kwa vijana; “Inavutia sio kwa sababu ni eneo ambalo nimekuwa nikilifanyia kazi, lakini ni vizuri kwa sababu ya kuandaa timu bora ya kesho.”
Kwa upande wake kocha wa timu za vijana wa Azam FC, Mohamed Badru alisema, “Ni hatua nzuri katika soka letu, tunatakiwa kuendelea kufanya kile tunachokiamini kwa ajili ya kuandaa mapema kikosi chetu cha timu ya Taifa, kuna mashindano makubwa yaliyo mbele yetu.”