JICHO LA MWEWE: Tulivyowaenzi Maradona na Pele kuliko Jellah Mtagwa

AMEZIKWA katika makaburi ya Kihonda, Ijumaa jioni baada ya swala ya Ijumaa. Jellah Mtagwa. Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars kuanzia mwaka 1973 hadi 1983. Miaka 10. Kuna heshima chache katika soka zaidi ya hii. Kuliongoza taifa lako katika vita kwa miaka 10. Hata hivyo, nani anamfahamu Jellah Mtagwa.

Mmoja kati ya walinzi bora wa kati kuwahi kutokea katika soka letu. Mmoja kati ya wachezaji wachache mahiri kuwahi kuandika historia zao katika kitabu cha soka la Tanzania. Mrefu kama alivyo, imara kama alivyo, alikuwa nguzo kubwa katika soka la Tanzania huku akiingia katika kikosi cha Stars kilichoshiriki kwa mara ya kwanza katika michuano ya Afcon mwaka 1980.

Kabla ya majuzi, mwaka 2019, wakati kina Mbwana Samatta na vijana wenzake walipotupeleka katika michuano ya Afcon pale Misri, kina Kaka Jellah na wenzake Leodeger Tenga, Aldoph Richards, Peter Tino na wengine walishatupeleka katika michuano ya Afcon mwaka 1980 ambayo ilifanyika Nigeria.

Unaweza kuhesabu mafanikio makubwa ya soka la Tanzania katika ngazi tofauti lakini kwenda Afcon Nigeria yalibakia kuwa mafanikio makubwa zaidi ya soka la Tanzania hadi kina Samatta walipoofanikiwa kwenda tena mwaka 2019. Jellah alikuwa roho katika mafanikio yake akiwa kama nahodha.

Amezikwa Ijumaa jioni Kihonda. Mara ya mwisho kumwona Kaka Jellah ilikuwa Machi 23, 2019 akiwa katika kiti cha wagonjwa cha kutembelea. Ajabu iliyoje. Alikuwa amekuja katika uwanja wa Taifa kutazama pambano kati ya Taifa Stars dhidi ya Uganda ambalo liliiwezesha Stars kufuzu michuano ya Afcon kwa mara nyingine baada ya miaka 39.

Kitu ambacho ni cha kawaida katika soka letu ni hakuna kijana aliyemwangalia mara mbili Jellah. Kila mtu alimpita kando na kuendelea na mambo yake huku akishangilia Stars kwenda Afcon Misri. Ambacho hawakukijua ni ‘mzee’ waliyekuwa wanampuuza ni Jellah Mtagwa ndiye aliyekuwa nahodha wa Taifa Stars wakati ikifuzu kwa mara ya kwanza kwenda Afcon mwaka 1980.

Wala hawakujua waliyekuwa wanamtazama ni mmoja wa mastaa wakubwa wa enzi hizo. Sawa, hakukuwa na Instagram, hakukuwa na Facebook, hakukuwa na mitandao ya kijamii. Hakukuwa na email. Njia kubwa ya mawasiliano wakati huo ilikuwa ni barua za kawaida. Ada pekee ya kupeleka barua ilikuwa ni stempu. Nchi nzima na katika picha za stempu aliwahi kuwekwa Jellah.

Ingekuwa zama hizi basi tungeweza kusema Jellah alikuwa mmoja kati ya watu waliokuwa kama Diamond Platinumz wakati huo. Sura yake ikitokea katika karibu kila barua ambayo ungeituma. Ni vile tu maandishi haya hayawezi kufikisha ujumbe halisi kwa kizazi kipya kwa namna Jellah Mtagwa alivyokuwa mtu mkubwa nyakati hizo. Staa wa kweli.

Kifo cha Jellah kimenifikirisha. Labda kwa sababu ya teknolojia lakini ukweli ni hatujarithisha vizazi vyetu kuwafahamu nguli halisi wa soka letu. Sio soka letu tu bali fani mbalimbali. Wazungu waliweza kuweka video mbalimbali za manguli wao na ingawa teknolojia haikuwa kubwa hivi lakini ilikuwa inaakisi kile walichokuwa wanafanya wakati huo.

Leo hii ukimzungumzia sana Jellah unaweza usieleweke. Watanzania asilimia 84 walizaliwa baada ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kufariki dunia mwaka 1999. Wanawezaje kumjua na kumheshimu Jellah? Ilipaswa turithishe vizazi vyetu kuwafahamu watu walioifanyia nchi hii mambo makubwa.

Ni vile tuliishi katika nchi masikini ambayo haikuwa na mambo ya video pamoja na kuweka kumbukumbu mbalimbali. Nchi ya kijamaa. Usinibishie. Mbona tuna kumbukumbu za picha na video za kina Diego Maradona, Pele, Johan Cruffy na wengineo? Ndiyo maana tuliomboleza vifo vyao kuliko kifo cha Jellah.

Tanzania ya leo iliwafahamu Maradona na Pele kuliko ilivyomfahamu Jellah. Sawa, wao walikuwa alama ya soka duniani, lakini bado mashabiki wa soka waliwafahamu mastaa wengineo wa ndani ya nchi zao. Sisi mastaa wetu wa zamani wa nchi yetu hatuwafahamu. Kinachoumiza ni hatukuwafahamu waliopita lakini huenda tusiwafahamu hata wa leo kama wakipotea.

Nani ni mchezaji aliyeichezea Taifa Stars mechi nyingi zaidi?  Nani ni mchezaji aliyekuwa nahodha wa muda mrefu zaidi kwa Stars? Nani ni mchezaji aliyeichezea Simba mechi nyingi zaidi? Nani ni mchezaji aliyeichezea Yanga mechi nyingi zaidi? Tunachokumbuka ni mchezaji aliyefunga hat trick katika mechi ya Simba na Yanga, King Abdalah Kibadeni. Kisa? Ni tukio la kipekee zaidi. Matukio mengineo hatuna rekodi nayo.

Mrisho Ngassa ni wa juzi tu lakini wengi wameshaanza kupoteza kumbukumbu zake. Kizazi kipya ambacho tunacho maisha yanaenda haraka kwao. Kama Ngassa anasahaulika vipi kwa Hamis Gaga? Kama Ngassa anasahaulika vipi kwa Nico Njohole? Tusiongee kabisa, hata Haji Manara anapomzungumzia baba yake Sunday Manara huwa tunadhani hasemi kweli. Kizazi kipya hakijui chochote kuhusu Sunday Manara.

Kuna mambo mawili ya kujifunza baada ya msiba wa Kaka yetu Jellah. Jambo la kwanza ni Jellah aliugua kwa muda mrefu sana. Unaweza kusema kwamba labda watu hawakujali sana lakini ukweli ni kwamba maisha ya kibepari ndivyo yalivyo. Kuna watu watasema kwamba hatuna mfumo wa kujali watu muhimu waliolitumikia taifa.

Inatufundisha kuishi maisha ya kibepari. Zipo nyakati ambazo Jellah alihitaji msaada. Ilionekana kama ni maisha yake binafsi na huo ndio ukweli. Ubepari unatufundisha kujijali. Hakuna anayekujali kama haujijajali. Ubepari unatufundisha ubinafsi. Unapopata nafasi ijali zaidi familia yako na maisha yako. Akina Kaka Jellah walifanya mambo mengi kwa ajili ya taifa, pia walipaswa kufanya mambo mengi kwa ajili yao.

Leo Ibrahim Bacca akihamia Simba kwa ajili ya kufuata masilahi mashabiki wa Yanga hawataweza kumwelewa hata kama dau la Simba lilikuwa juu lilikuwa kubwa kuliko la Yanga. Ni hivyo hivyo ambavyo kama Mohammed Hussein Tshabalala akihamia kuhamia Yanga kwa ajili ya kufuata masilahi. Kisa? Tunaamini wachezaji wanapaswa kuwa mashabiki. Sio sawa.

Wanapougua wanakuwa peke yao. Mpira unapoisha katika miguu yao wanakuwa peke yao. Ni kama watu wa fani nyingine tunapoamua kujali maslahi yetu binafsi. Labda kina Kaka Jellah walijali masilahi ya watu wengine kuliko masilahi yao binafsi, ndiyo maana walihitaji michango yetu wakati walipougua.

Msiba wa Jellah pia unatufundisha kuweka kumbukumbu kwa ajili ya vizazi vyetu. Labda hatujachelewa sana. Watu wa takwimu wawe bize kweli kweli na mastaa wa sasa wa fani tofauti. Watasababisha tuwaheshimu akina Jellah wapya pindi watakapoondoka duniani. Inakera kidogo kuona tofauti kubwa ya namna wenzatu wanavyoheshimu watu wao waliofanya mambo makubwa zamani tofauti na sisi tulivyofanya kwa Jellah.

Ni wazi kuna watu walipata uchungu mkubwa wa kifo cha Maradona kuliko Jellah. Kifo cha Pele kuliko Jellah. Kifo cha Marc-vivien Foe kuliko Jellah. Kumbe kama watu wengi wangefundishwa kumjua Jellah wangeumia zaidi. Hatujachelewa sana. Tumjue Samatta na kuendelea kumweka katika ramani hata baada ya miaka mingi ijayo.

Related Posts