Kampeni wagombea Chadema zashika kasi kwenye kanda

Dar es Salaam. Wagombea wa nafasi mbalimbali kwenye kanda nne ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamesema uchaguzi utakaofanyika kati ya Mei 25 na 29, 2024 hautakuwa mwepesi kwa sababu kwa asilimia kubwa umewakutanisha wagombea waandamizi wa ndani ya chama hicho.

Wamesema uchaguzi huo utakuwa na ushindani, tofauti na mwingine wowote awali, kwa sababu unawakutanisha wagombea waliowahi kufanya kazi pamoja kwa nyakati tofauti, katika kanda na Kamati Kuu ya Chadema.

Wameeleza hayo leo Jumapili Mei 19, 2024 wakizungumza na Mwananchi iliyotaka kujua mipango mikakati siku mbili baada ya kamati kuu ya chama hicho, iliyoketi Mei 11 hadi 14, 2024 kupitisha majina yao.

Kanda zitakazofanya uchaguzi ni Serengeti yenye mikoa ya Mara, Shinyanga na Simiyu, Magharibi (Tabora, Katavi na Kigoma), Nyasa (Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe na Rukwa) na Victoria (Mwanza, Kagera na Geita).

Mgombea uenyekiti wa Kanda ya Victoria, John Pambalu amesema mchakato wa kanda hizo hauwezi kuwa rahisi, utakuwa wa ushindani kwa sababu umekutanisha vigogo ambao ni wazoefu ndani ya chama hicho.

“Mfano katika kanda yetu kuna mwenyekiti anayetetea nafasi yake (Ezekia Wenje) na mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) wote ni wajumbe wa kamati kuu. Uchaguzi huu utakuwa mgumu maana unashirikisha watu wazito wao kwenye siasa wanafahamika.”

“Kanda ya Serengeti inakutanisha makamu mwenyekiti wa sasa na kaimu mwenyekiti wa kanda (Gimbi Masaba) na Lucas Ngoto aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mara kwa muda mrefu,” amesema Pambalu.

Amesema katika Kanda ya Magharibi ina mwenyekiti anayetetea muda wake na mwenyekiti aliyewahi kuongoza kanda ya hiyo na wengine waliobaki ni watu waandamizi ndani ya chama, akiwemo Wakili Dickson Matata.

Katika kanda ya Nyasa, Pambalu amesema inawakutanisha Joseph Mbilinyi’ Sugu’ ambaye ni mjumbe wa zamani wa kamati kuu na Mchungaji Peter Msigwa anayetetea kiti chake kwa awamu ya tatu.

“Maisha yangu ya kisiasa ya miaka 14 ndani ya Chadema hizi ndio chaguzi za kanda zenye ushindani mkubwa zaidi, haijawahi kutokea chaguzi zenye ushindani kama hizi hii inaonyesha ukuaji wa chama hiki,” amesema.

Hata hivyo, Pambalu amesema anaomba kura kutokana historia yake ndani ya Chadema, akisema atatumia uzoefu wake wa uongozi wa Bavicha kufanikisha mchakato huo. Amesema ameongoza baraza la vijana katika mazingira magumu lakini amefanikiwa.

“Nimewaongoza vijana kuandika sera ya Taifa ya vijana, kupigania uhuru wa viongozi wetu waliokamatwa baada ya uchaguzi 2020, kudai Katiba Mpya. Pia sera zangu endapo nitaibuka kidedea zinaeleweka na nimetumia lugha nyepesi kufikisha ujumbe, ikiwemo kujikita katika mafunzo kwa viongozi,” amesema Pambalu.

Mchungaji Peter Msigwa amesema joto la uchaguzi kwenye Kanda yake ya Nyasa linaenda kawaida na anajiona atashinda kwa kishindo kikubwa huku akieleza wasifu wake wa kufanya kazi iliyotukuka kuwatumikia wananchi bila kuchoka kutamsaidia.

“Nimekuwa kiongozi wa kanda hii kwa awamu mbili. Nimefanya kazi kubwa kwa kuja na sera mbadala kushindana na Chama cha Mapinduzi (CCM). Lakini najua kujenga hoja najiona nashinda mapema kabisa,” amesema.

Mchungaji Msigwa amesema hata kampeni zake anafanya kisasa, hazunguki na msafara wa magari mengi kwani alipokuwa kiongozi alifanya vikao vingi, hivyo kazi nzuri alizofanya zitamsaidia.

“Saa hizi naongea na wewe nipo Chimara kwenye Mwang’ombe Cup. Kifupi kampeni nimeanza lakini siwezi kutembea na magari kama kwenye mikutano ya hadhara,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu mpinzani wake, Mchungaji Msigwa amejibu ni kiongozi mzuri lakini hawawezi kushindana katika uchaguzi huo kwa kuwa anamzidi kwa mengi.

Sugu ambaye ni mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, amesema “uchaguzi huu wapiga kura wake sio wale wa umma, bali wapo ndani ya chama. Katika kanda yetu wapigakura hawazidi 120, nimeshaandaa njia za kuwafikia kama sehemu ya kuanza rasmi kampeni za kuomba au kuthibitisha.”

Mgombea nafasi ya umakamu mwenyekiti Kanda ya Nyasa, Frank Mwakajoka amesema joto la kampeni hizo ni nzito na linachagizwa na wasifu mzuri wa wapinzani waliojitokeza katika mchakato huo.

“Joto ni nzito, uchaguzi ni uchaguzi ilimradi matarajio yangu ni kushinda na kuongoza kanda na watu wananiamini kutokana na maono niliyonayo ni makubwa,” alisema.

Kuhusu ushindani na hoja ya wasifu mzuri wa wapinzani wake, Mwakajoka amesema hawezi kuwabeza wapinzani wake kwa sababu wana rekodi za uadilifu walipopewa fursa ya kuongoza nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho.

“Ni viongozi wazuri wamekitumikia chama vizuri kwa wakati wote na katikati yetu hakuna ambaye hajawahi kuwa kiongozi, lakini nimewahi kushika nyadhifa kadhaa hadi ubunge na mwenyekiti wa wilaya, wote tuko vizuri,” alisema.

Mwakajoka amesema kwa kuwa huo ni uchaguzi na anatakiwa kupenya mmoja, hakuna anayedhani anapenda mwenzake ashinde na mwenyewe abaki.

“Naamini napambana nishinde na nitashinda na nina vigezo zaidi ya wenzangu, wote tuko vizuri lakini nawazidi pakubwa kwa sababu ya malengo makubwa ninayotaka kuifanyia Kanda yetu,” amesema Mwakajoka.

Amesema akitangazwa ameshinda nafasi hiyo jambo la kwanza ataimarisha amani na mshikamano huku akieleza uwezo wake wa kushauri na kuwajaza watu uvumilivu unaompa jeuri.

Gimbi Massaba anayewania uenyekiti Serengeti amesema uchaguzi huo ni mgumu na wala si mrahisi, hivyo maarifa na juhudi zinahitajika kushawishi wanachama wawachague viongozi wanaowahitaji.

“Wanakwambia uchaguzi ni uchaguzi kaka, hakuna uchaguzi rahisi. Hatufanyi kampeni za kuumizana tukiamini kwamba baada ya uchaguzi kuna maisha mengine yanapaswa kuendelea, kikubwa tunatafuta mwakilishi,” amesema

Katika maelezo yake, Massaba amesema shabaha yake ni kupata ridhaa ya kuongoza kanda hiyo ingawa haiwezi kuwa rahisi kwani mpinzani wake Ngoto naye amejipanga.

“Nilishaanza kampeni mkoani Shinyanga lakini saa hizi naelekea Simiyu. Mpango wangu kuongoza kanda na kuiunganisha kuwa kitu kimoja na kufuta makundi mbalimbali,” amesema.

Amesema atahakikisha anafuta makundi kwa kuwa mchakato wa uchaguzi mara nyingi huwa unaacha majeraha.

“Baada ya hapo nitaanza mkakati wa kututoa tulipo katika kukabiliana na uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwakani,” amesema.

Hata hivyo, Masaba amesema ikitokea ameshindwa kwenye mchakato huo atakuwa tayari kumuunga mkono mshindani wake ili kuondoa mpasuko unaoweza kujitokeza ndani ya chama.

“Sitaki kuwa sehemu ya kukipasua chama ambacho ninakipenda na kimenilea lakini pia kilinipa heshima ya kuwa makamu mwenyekiti wa kanda na kaimu mwenyekiti wa kanda ya Serengeti,” amesema Masaba.

Kwa upande wake mshindani wake Ngoto, amesema baada ya kuanza kampeni za awali, anaona ushindi ni asilimia 70 na kwa kushirikiana na timu yake wanapambana kufikisha asilimia 90.

“Sina mashaka na mpinzani wangu, unajua amekuwa kwenye nafasi hiyo kwa kukaimu kwa muda mrefu hivyo naona kumshinda ni rahisi kwa kuwa najua mapungufu yake,” amesema.

Ngoto amesema malengo ya chama chochote cha siasa ni kushika dola hivyo baada ya kutangazwa mshindi shabaha yake itajikita katika suala hilo.

“Malengo yangu ni kuhakikisha chama chetu kinashika dola na tunajua tuna uchaguzi wa mitaa na uchaguzi mkuu mwaka ujao. Nina rekodi nzuri ya kusimamia chaguzi hizi mfano mwaka 2014 nilipokuwa mwenyekiti wa Tarime tulishinda mitaa 50.

“Katika viiji 88 vilivyopo Tarime tuliongoza vijiji 39, uzoefu huo nategemea kuambukiza kanda yetu kuhakikisha mikoa yote inafanya vizuri. Mwaka 2015 tulichukua majimbo yote Tarime Mjini na Vijijini,” amesema.

Related Posts