Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema kimbunga Ialy kinachovuma kaskazini mwa kisiwa cha Madagscar, ambacho awali kilidaiwa kingeishia baharini, kinaendelea kupata nguvu na kinatarajiwa kusababisha mvua kubwa na upepo mkali Tanzania siku ya Jumanne Mei 21, 2024.
Taarifa iliyotolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi leo Jumapili Mei 19, 2024 imesema kuwa TMA katika taarifa yake ya saa 12 jioni ya leo, imetabiri kimbunga hicho kilichopo umbali wa kilomita 680 kutoka pwani ya Tanzania, kuwa kitasababisha mvua kubwa na upepo mkali Jumanne.
“Hali hiyo itasababisha upepo mkali baharini unaozidi kasi ya kilomita 40 kwa saa na mawimbi yanayozidi mita 2 hadi Jumanne, Mei 21 huku mvua kubwa ikitabiriwa kunyesha katika maeneo ya pwani ya nchi yetu kati ya Jumanne, tarehe 21 na Jumatano, tarehe 22 Mei, 2024,” imesema taarifa hiyo.
Aidha, taarifa hiyo imesema watumiaji wa bahari na wananchi wanashauriwa kuchukua tahadhari na kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa.
Kabla ya tishio hili la kimbunga Ialy, Mei 1, 2024, TMA ilitoa tahadhari ya kuwapo kwa kimbunga Hidaya ambacho baadaye kilikosa nguvu baada ya kuingia pwani ya Bahari ya Hindi na kusababisha madhara machache ikiwemo mvua kubwa ya upepo katika maeneo ya Mafia, Mtwara na Kilwa.
Kwa mujibu wa tovuti ya Zoom Earth, Kimbunga Hidaya kilianza Aprili 28 karibu na Visiwa vya Ushelisheli kikiwa na mwendokasi wa kilomita 30 kwa saa.
Aprili 29 kiliongezeka kasi na kufikia kilomita 35 kwa saa huku kikiwa bado na nguvu kadiri, kiliendelea kujikusanya zaidi hadi Aprili 30 saa 3.00 usiku kikafikia kasi ya kilomita 45 kwa saa.
Mei 1 kiliendelea kusogelea Pwani ya Bahari ya Hindi huku kasi ikiongezeka hadi kilomita 65 kwa saa na hapo ndipo Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ikatoa tahadhari ya uwapo wa Kimbunga Hidaya.
Kikiwa kinaendelea kuisogelea Pwani ya Bahari ya Hindi, Mei 2 kiliendelea kuimarika zaidi na kufikia kasi ya kilomita 120 kwa saa hadi saa 3.00 usiku.
Mei 3, 2024 hadi saa 3 asubuhi kasi yake iliongezeka zaidi na kufikia kilomita 150 kwa saa, huku baadhi ya maeneo ya pwani ya Bahari ya Hindi yakianza kupata madhara. Mpaka saa 9 mchana, Mei 3 kimbunga Hidaya kilianza kuikaribia Tanzania huku kikipungua kasi hadi kufikia kilomita 110 kwa saa.
Mei 4 kimbunga Hidaya kilitua katika Kisiwa cha Mafia kikiwa na kasi ya kilomita 95 kwa saa na kusababisha madhara kadhaa kama kuangusha miti, miundombinu ya umeme na mvua kubwa.
Mei 5 kiliifikia Tanzania hususani mikoa ya Lindi, Mtwara na Morogoro kilipungua nguvu hadi kilomita 55 kwa saa na kuwa cha kawaida kisichosababisha madhara.