Dar es Salaam. Wakati wanatasnia ya dawa na Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) wakiomboleza kifo cha Mansoor Daya, mwanzilishi wa biashara ya dawa nchini na Afrika Mashariki, mchango wake umetajwa akuwa mkubwa ambao hautasahaulika.
Daya ni mfamasia wa kwanza kusajiliwa na Baraza la Famasi nchini ambalo hadi mwaka 2023 limesajili wafamasia 2,996, fundi dawa sanifu 4,518 na fundi dawa wasaidizi 787.
Wengi tumekuwa na mazoea ya kwenda maduka ya dawa maarufu famasi kununua dawa, lakini historia inaonyesha kabla ya uhuru kulikuwa na famasi tatu pekee katika mkoa wa Dar es Salaam, moja Morogoro na nyingine ilikuwa Arusha.
Mwanzilishi huyo wa famasi nchini, aliyefariki dunia Alhamisi Mei 16, 2024 jijini Dar es Salaam akiwa na umri wa miaka 93, ameacha alama ambazo hazitasahaulika, kwa mujibu wa wadau wa viwanda na dawa nchini.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha wamiliki wa viwanda vya dawa nchini, Churchill Katwaza Mansoor Daya alizikwa jana kwenye makaburi ya Kijitonyama.
Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI) limemtaja Mansoor Daya kama kiongozi aliyekuwa na msukumo, aliyejitolea maisha yake kwa ukuaji na mafanikio ya kampuni yake na sekta ndogo ya dawa kwa ujumla.
“Tunapongeza kujitolea kwake bila kuyumbayumba kwa ubora, uvumbuzi na jukumu lake muhimu katika kukuza ukuaji wa viwanda nchini,” ilieleza taarifa ya CTI iliyotolewa Ijumaa Mei 17, 2024.
Katika mahojiano na Mwananchi mwaka 2018, Daya alieleza maono yake kwenye viwanda vya ndani, kuwa vinapaswa viongeze uwezo na kutosheleza soko la ndani.
“Tuongeze uwezo wa viwanda vya ndani. Tutosheleze soko na tukiuza nje viwanda vitanufaika na nchi itaingiza fedha za kigeni.”
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, wafamasia na wataalamu wa dawa nchini wamemwelezea Daya, namna alivyopambana kuhakikisha tasnia hiyo inasimama nchini.
Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi amesema kifo cha Daya aliyeanzisha kiwanda cha bawa wakati wa Uhuru, pamoja na kwamba ni pigo kwa familia, ni pigo kwa taifa kutokana na maono aliyokuwa nayo ya kupunguza uagizaji wa dawa kutoka nje ya nchi.
Amesema kifo chake ni pigo kwa wanaharakati wote wenye mikakati ya kuanzisha uzalishaji wa dawa nchini, kwani kuna vitu vingi vya kujifunza kutoka kwake na kuwa kikubwa ni kuziishi ndoto zake.
“Ndoto aliyotamani itokee ni aone Tanzania ina uzalishaji wa dawa wa kutosha ili kupunguza utegemezi kutoka nje. Akiwa Katibu na mwenyekiti wa chama cha wazalishaji dawa Tanzania, amekuwa ni msaada kuonyesha maeneo yenye changamoto, kusaidia kuonyesha njia, ‘hapa kuna shida, tufanye hivi na hivi kwa ajili ya kuboresha.’
“Amekuwa mzalendo wa kweli, wengi waliwekeza nje lakini yeye aliwekeza ndani, muda wote viwanda vyake vinafanya kazi ya uzalishaji, muda wote amekuwa mtu wa msaada,” amesema Msasi.
Msajili wa Baraza la Famasi nchini, Boniface Magige amesema Daya alikuwa ni dira kwa sababu ya mchango wa taaluma kwa kuanzisha kiwanda cha dawa, tofauti na wafamasia wengi ambao wakihitimu elimu yao, huenda kufungua maduka ya dawa.
“Kiwanda ndiyo sehemu kubwa ya taaluma ya dawa na kiwanda ndiyo mchango wa kutoa huduma ya dawa itakayomtibu mtu, mchango wake ulikuwa kuiweka taaluma katika eneo la kimataifa, unapokuwa na kiwanda ukauza ndani na nje ya nchi unasaidia jamii kubwa zaidi,” amesema Magige.
Mfamasia Levu Mhangwa amesema Mansoor Daya atakumbukwa daima kwani wanafunzi wa kada hiyo walitumia kiwanda chake kujifunza kwa vitendo.
“Nilipohitimu Kikuu Kishiriki cha sayansi na tiba Muhimbili (Muhas) mwaka 1977 nilienda kusoma nje, huko nilikuwa tayari najua kiwanda cha dawa kikoje, nilishakiona na uzalishaji pia. Isingekuwa Mansoor Daya ningeenda sina hiyo elimu,” amesema Mhangwa ambaye pia amekuwa mhadhiri wa kada hiyo na mkaguzi wa viwanda vya dawa.
Amesema Daya alikuwa wa kwanza kufungua maduka ya dawa nchini, kwa kabla ya uhuru kulikuwa na matabaka matatu, la walio nacho, tabaka la kati na wengine waliotibiwa katika vituo vya afya.
“Famasi zilikuwa kama tatu Dar, Morogoro moja na Arusha moja kabla ya uhuru, yeye aikiwa mwanzilishi. Mwaka 1962 akaanzisha kiwanda cha dawa pekee mpaka Shellys walipozindua kiwanda Pugu Road (Barabara ya Nyerere) ndio kikawa cha pili,”
Amesema Daya aliendelea kutanua wigo wake wa kutengeneza dawa na ndiyo kiwanda pekee ambapo waliosoma tasnia ya dawa walienda kujifunza kwa vitendo, kabla ya Serikali kujenga kiwanda chake Arusha.
“Alishikilia uzalishaji bila kukata tamaa, pamoja na misukosuko mingi ya kiuchumi kiwanda chake hakijawahi kusimamisha uzalishaji. Angeweza kuacha, kwani ni biashara ambayo wengi wanaiogopa, dawa ikienda sokoni bado ni yako mpaka mtumiaji wa mwisho bado ni yako, ikileta shida ni wewe,” amesema.
Hadi anafariki, Mansoor Daya aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Mansoor Daya Chemicals Limited ya jijini Dar es Salaam.
Kiwanda hicho, chenye historia ya zaidi ya miaka 60 katika uzalishaji wa dawa nchini, awali kilisambaza dawa kwa nchi jirani kama Kenya, Uganda, Burundi na Zambia. Hata hivyo, baadaye kilijikita katika kuhudumia soko la Tanzania.
Chini ya uelekezi na mwongozo wake, Mansoor Daya Chemicals Limited, ilipanua bidhaa zake hadi takriban 50 za dawa na hivi karibuni ilianzisha dawa za asili ili kuongeza uwezo wa kumudu bei kwa watu wengi. Kiwanda chake kilichoanza mwaka mmoja baada ya uhuru kilianza kwa aina nne za dawa.