Mchakato mrefu unavyowakosesha bodaboda wengi leseni

Dar/mikoani. Mchakato mrefu wa upatikanaji wa leseni za udereva kwa madereva wa pikipiki na bajaji pamoja na tozo za Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (Latra), vimetajwa kuwa chanzo cha uendeshaji holela wa vyombo hivyo.

Hayo pia yanatajwa kuwa miongoni mwa sababu za madereva wengi wa pikipiki maarufu bodaboda kutokuwa na mafunzo wala leseni za udereva, hivyo kuchangia ongezeko la ajali za barabarani zinazosababisha majeruhi na vifo.

Takwimu za mwaka 2023 za Wizara ya Mambo ya Ndani zinaonyesha asilimia 40 ya ajali zinazotokea nchini husababishwa na bodaboda.

Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) mwanzoni mwa mwaka huu imeeleza asilimia 60 ya majeruhi wanaopokewa idara ya dharura hospitalini hapo wanatokana na bodaboda.

Takwimu za MOI zinaonyesha, takribani majeruhi 20 hadi 25 hupokewa kwa siku kwa ajili ya matibabu.

Akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2024/25 bungeni jijini Dodoma Mei 6, 2024, Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby alisema licha ya asilimia 95 ya bodaboda kutokuwa na leseni, mfumo uliopo unawanyanyasa.

Shabiby alihoji sababu ya Latra kuwalipisha bodaboda Sh17, 000 kila mwaka akisema ni unyanyasaji.

“Mnachukua Sh17, 000 kwa mwaka kwa bodaboda, lakini ninyi hamumpangii ruti, anatafuta mwenyewe, usiku kucha anahangaika mwenyewe,” alisema.

Kuhusu leseni, Shabiby alihoji sababu ya madereva wa pikipiki kulipishwa Sh70, 000 sawa na madereva wa magari.

“Bodaboda leseni yao ni Sh70, 000, ili apate lazima akasome chuo Sh50,000. Kwa hiyo gari la miguu minne na ile pikipiki yenye miguu miwili leseni yake ni moja Sh70, 000 inawezekana wapi hii?”

“Kwenye bodaboda, leo asilimia 95 ya madereva hawana leseni. Kwa hiyo, mnatunga sheria mnatunga utaratibu ambao hautekelezeki,” alisema Shabiby.

Alishauri leseni kwa madereva wa bodaboda iwe Sh25, 000 hadi Sh30, 000 akitoa mfano wa mabadiliko ya Sheria ya Usalama Barabarani iliyobadilisha faini kwa madereva hao kutoka Sh30,000 kuwa Sh10,000.

Mkurugenzi wa Latra, Johansen Kahatano amekiri kuwatoza madereva wa pikipiki tozo hizo ikiwa ni utekelezaji wa kanuni ya vyombo vya kukodi ya mwaka 2020 inayohusisha pikipiki na bajaji.

“Kwa kanuni hizi, mamlaka inatoza ada ya Sh15,000 kwa pikipiki na Sh2,000 ni ya usajili, hivyo inakuwa Sh17,000. Kwa bajaji ada ni Sh20,000 na Sh2,000 ni kwa ajili ya maombi,” amesema.

Kahatano amesema ada hizo zilipunguzwa, awali ilikuwa Sh20,000 kwa pikipiki na Sh30,000 kwa bajaji.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, baadhi ya madereva wa pikipiki wameeleza mchakato wa kupata leseni ni mgumu.

Baadhi ya viongozi wa waendesha bodaboda mkoani Dodoma wamesema idadi kubwa ya madereva hawana leseni za udereva.

William Mdache, mwenyekiti wa kijiwe cha waendesha bodaboda Bahi Road, amesema kuna kundi kubwa la vijana wanaoendesha bodaboda pasipo kuwa na leseni, wakikwepa mchakato mrefu wa mamlaka za Serikali unaowataka wakasome na pia kulipia gharama kubwa.

“Kijiwe changu kina wanachama 25 wenye leseni hawazidi wanne. Tumewaambia wasipopata leseni wakipata changamoto yoyote barabarani ikiwamo ajali hawatapata msaada,” amesema Mdache.

Amesema inapowalazimu kuwa na leseni, baadhi hutumia njia zisizo rasmi.

“Hela ndiyo kila kitu ukiwa na Sh200,000 unapata leseni unayoitaka, kwa hiyo hata hao walionazo hawajapita kwenye vyuo vya udereva bali wamezipatia mitaani,” amesema Mdache.

Raphael Kamate, mwenyekiti wa kijiwe cha bodaboda Makulu Stendi amesema wameweka utaratibu wa wanachama wanaojiunga kijiweni hapo lazima wawe na leseni.

Amesema hilo linatokana na taarifa ya majina ya wanachama kupelekwa vituo vya polisi, hivyo ni lazima namba ya leseni ya dereva iwepo.

Jackson Mwakasiga anayefanya kazi Mtaa wa Sokoine amesema anatamani kuwa na leseni lakini anashindwa kutimiza masharti.

“Nashauri gharama za leseni zibaki vivyo hivyo, lakini suala la kuwa na vyeti liondolewe kwa kuwa ni ngumu, zamani tulitumia kampuni kupata leseni, sasa lazima RTO (Kamanda wa Polisi Usalama Barabarani wa Mkoa) ndiye aidhinishe,” amesema Mwakasiga.

Utaratibu wa kupata leseni

Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mbeya, Princepius Nshangeki amesema ili kupata leseni lazima dereva awe na cheti cha mafunzo ya udereva, namba ya TIN (Namba ya Mlipakodi), na kitambulisho cha Taifa (Nida).

Amesema katika kukamilisha mchakato wote, mteja atalipia Sh83,000 kati ya hizo, Sh70,000 ni za ada ya leseni ambayo inadumu kati ya miaka minne hadi mitano, Sh10,000 ya ufundishaji na Sh3,000 ya majaribio.

“Sisi hatuna masharti makubwa na kwa sasa tumetoa muda kuanzia Mei hadi Juni bodaboda wote wasio na leseni waje wapate huduma, hakuna adhabu yoyote wataipata,” amesema.

Meneja Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Paul Walalazo amesema namba ya TIN itamsaidia kuingizwa kwenye mfumo wa kuanza mafunzo na kupata leseni.

Amesema mafunzo hutolewa kwenye vyuo vya udereva na dereva anapohitimu hupatiwa cheti ambacho humtambulisha aina ya daraja analopaswa kupatiwa leseni.

“Akija TRA atapewa fomu ya kujaza na kuingiziwa madaraja, baada ya hapo tunamtuma kwa mtu anaitwa vehicle inspector ‘mkaguzi wa vyombo vya moto’ na huko atakwenda kutathiminiwa kama kweli anamudu kuwa dereva na majibu yake kutumwa TRA,” amesema Walalazo.

Walalazo anasema baada ya dereva kuthibitishwa, TRA hupatiwa namba ya malipo ya Sh70,000 ambayo ni gharama ya leseni atakayodumu nayo kwa miaka mitano.

Hata hivyo, Kamanda wa Usalama Barabarani Jiji la Mbeya, Komba Ansigai anakanusha uwepo wa masharti magumu kupata leseni.

“Wanachopaswa kufanya ni kusoma, wawe na vyeti ili wafike TRA wawasilishe taarifa zao wapewe leseni, sisi trafiki tunafanya kazi kwa mujibu wa sheria,” amesema Kamanda Komba.iashara ngumu

Faustine Jerome, bodaboda katika Mtaa wa Sangu jijini Mbeya amesema biashara hiyo haina uhalisia kuna nyakati wateja wanapatikana na zingine hawapatikani.

Joram Munuo dereva bodaboda eneo la Tabata Mwananchi jijini Dar es Salaam, amesema mwaka 2018 kwa siku mtu aliweza kuingiza Sh120,000 kwa kuwa walikuwa wachache, lakini kuanzia mwaka 2020 hadi sasa hali ni tofauti  kutokana na wengi kuendesha bodaboda.

Amesema kijiwe chao sasa wapo 120 tofauti na madereva sita waliokuwepo kuanzia mwaka 2018, na  kwa siku unaweza kupata Sh20,000.

“Kiwango hicho ni kwa mtu aliyeamka saa 10.00 alfajiri na kufanya kazi hadi saa 12.00 jioni,” amesema.

Changamoto ya kipato, elimu na rushwa vinatajwa kuwa miongoni mwa sababu za madereva kukosa leseni za udereva.

“Mchakato wa kupata leseni ni mzuri ila tunaomba uboreshwe kwa sababu kwetu sisi bodaboda ukianza kufuatilia inachukua wiki moja hadi mbili, tunaomba angalau mchakato uwe wa siku moja au mbili ukizingatia waendeshaji wa vyombo hivyo ni wengi,” amesema Joel Alexander dereva bodaboda katika Kituo cha Barabara ya Rufiji jijini Mwanza.

Abeli Urio yeye amedai uwepo wa baadhi ya watumishi au maofisa kuwataka madereva kutoa rushwa ili kupatiwa leseni imekuwa ikisababisha wengi wao kuacha kufuatilia leseni.

Mkoani Arusha baadhi ya madereva wameeleza kutokana na mafunzo wanayopata kila mara hasa usalama barabarani na kutambua vihatarishi vya ajali, asilimia kubwa wana leseni.

Kaimu Katibu wa Umoja wa Bodaboda Mkoa wa Arusha, Hakim Msemo amesema wameanzisha mfumo wa takwimu miezi miwili iliyopita kwa lengo la kutambua madereva wote mkoani humo kubaini wenye leseni na ambao hawana.

“Tumetengeneza mfumo wa data kwa Jiji la Arusha tunakadiria wapo zaidi ya 12,000 na hadi sasa waliojisajili kwenye mfumo ni zaidi ya 6,000 ambao tumewapitia kwenye vituo vyao na kuchukua taarifa zao,” amesema.

Katika udhibiti wa ajali za bodaboda, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Ramadhani Ng’anzi amesema hatua wanazoendelea nazo ni kutoa elimu kwa kundi hilo juu ya kuzingatia usalama barabarani.

Mkurugenzi wa Barabara wa Latra, Johansen Kahatano amesema mabadiliko ya Sheria ya Usafirishaji na kanuni zake zimewapa mamlaka ya kutoa leseni za biashara hiyo badala ya halmashauri za wilaya. Ili kutekeleza mamlaka hayo, amesema wameshaingia makubaliano na halmashauri 119 kati ya 184 kwa ajili ya usajili wa bodaboda na bajaji. Kati ya hizo 78 ndiyo zinatekeleza makubaliano hayo.

Hata hivyo, amesema kanuni zinaruhusu Latra kutoa kibali kwa mamlaka za mitaa (halmashauri), kampuni binafsi na vyama vya ushirika.

Imeandikwa na Baraka Loshilaa (Dar) Saddam Sadick (Mbeya), Rachel Chibwete (Dodoma), Janeth Mushi (Arusha) na Anania Kajuni (Mwanza)

Related Posts