Mtandao wa kuomba ajira Polisi walalamikiwa haufunguki

Dodoma. Wakati siku ya mwisho ya maombi ya kazi kwenye Jeshi la Polisi ni Jumanne ya Mei 21, 2024, waombaji wengi wamelalamikia mtandao wa jeshi hilo kutofunguka.

Malalamiko hayo yametolewa na watu mbalimbali huku wengine wakishauri jeshi hilo liruhusu barua za maombi zipelekwe kwa mkono kwa makamanda wa polisi wa mikoa na wilaya.

Malalamiko ya watu hao yako kwenye maoni ya taarifa za polisi  kwenye akaunti yao ya ‘Police Force TZ @tanpol’ iliyopo kwenye mtandao wa X.

Mei 15, 2024, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alitangaza kuongeza siku tano  za kuomba ajira kwenye Jeshi la Polisi ambazo siku yake ya mwisho awali ilikuwa Mei 16, 2024.

Masauni alisema hayo baada ya kutolewa hoja na Mbunge wa Makete, Festo Sanga aliyetumia kanuni namba 54 ya kutoa jambo la dharura bungeni, kwamba kukosekana kwa mtandao wa intaneti nchini (wakati huo) kungewakosesha fursa vijana kwa kushindwa kutuma maombi ya kazi.

Licha ya kuongezwa siku tano, Masauni pia alisema iwapo changamoto ya intaneti itaendelea, Serikali itaangalia namna ya kufanya ili kuwasaisia waombaji kufikia lengo.

Malalamiko yaliyopo kwenye maoni ya taarifa za polisi anasema;   ‘Hivi ‘link’ ya ajira itaanza kufunguka lini? Na siku ndo zinakaribia kuisha’ ameandika LYRICIST@EngsJohn. Mwingine joEAGGY 🌗@JoeAggy22 anasema ‘Anii shida tu’. Pia, cole@coheleth_yeye anasema ‘Mfumo bado changamoto. Na hamtoi taarifa yoyote shida nini?

Mwingine CIA@CiaMwana yeye anasema; ‘link ya kutuma maombi haifunguki sisi tulio na internet cafe wateja hawatuelewi, wanadhani tunawatapeli, toeni hata neno kwamba mfumo wenu umeshindwa kukabiriana na changamoto iliyojitokeza, mtusaidie, wateja wanatuona wezi wa kimtandao kwa hiki kinachoendelea.’

Mlalamikaji mwingine @MpunjoSaid yeye anasema ‘Hizi siku mlizoongeza ili watu wafanye maombi ni bora mngeziongeza baada ya kufanya marekebisho ya mtandao wenu kwanza. Siku zinaisha changamoto inaendelea kuwepo what is this (Hii nini nini)?

Mlalamikaji mwingine @WokaSky anasema, ‘Wakuu mfumo haujakaa sawa kabisa unagoma kabisa kufunguka.

Mwingine @MbweleJohn anasema ‘Mfumo wa maombi ya ajira unagoma kufunguka, fanyeni namna ya kurekebisha hili.’

Related Posts