Same. Unaweza kuwa ni moja ya miamba ya aina yake kuwahi kuonekana nchini Tanzania unaopatikana katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, unaoonekana kama taswira ya binadamu.
Pamoja na mwamba huo wenye taswira ya mwanaume, pembeni yake, kushoto na kulia, zipo taswira mbili za wanawake wanaoonekana ni wajauzito.
Mwamba huo uliopewa jina la “Ikambalafua” kwa kabila la Wapare ikimaanisha “mwamba wa pua”, umekuwa ni wa kihistoria na kivutio cha watu wengi kutoka ndani na nje ya Kijiji cha Kambeni, kata ya Myamba.
Akizungumzia mwamba huo, mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Yohana Ramadhani (70), amesema mwamba huo umekuwa ni maarufu kijijini hapo na maeneo mengine ya jirani kutokana na mwonekano wake.
Amesema mwamba huo ambao upo karne na karne ungetumiwa vizuri kama kivutio cha utalii, kijiji hicho kingepata mapato kutokana na mwonekano wa namna miamba ilivyoumbwa.
“Ukiangalia huu mwamba, huyu bwana yupo katikati na wanawake wawili ambao wapo pembeni yake, wote wana mimba, yaani ni maajabu ya Mungu, tulizaliwa na tuliukuta hivyo, umekuwa ukitumika kama sehemu ya utalii,” anasema.
Mkazi mwingine wa Myamba wilayani humo, John Gosso amesema mwamba huo umekuwa ni wa kipekee katika eneo hilo kutokana na namna eneo hilo lilivyojijengea umaarufu wake.
“Mwamba huu wa kihistoria upo tangu enzi na enzi lakini hatujaona manufaa yake. Tunaomba Serikali ifanye utaratibu wa namna ambavyo wananchi tutanufaika nao, ikiwezekana watengeneze uwe ni miongoni mwa vivutio rasmi vya utalii hapa Same,” amesema.
Akizungumzia mwamba huo, Ofisa Michezo, Sanaa na Utamaduni, Wilaya ya Same, Nevlin Nyange amesema Serikali itaangalia namna ya kukiweka kivutio hicho kuwa ni miongoni mwa vivutio vya asili vinavyopatikana wilayani humo, ili pia wananchi wanaoishi katika maeneo hayo wanufaike na uumbaji huo.
Nyange amesema hilo litasaidia kijiji kupata mapato yake ya ndani na halmashauri na baadaye Taifa, kama ilivyo katika vivutio vingine vya asili vilivyopo katika maeneo mengine nchini, kama vile kimondo kilichopo mkoani Mbeya.
Amesema wilaya hiyo imekuwa na vivutio mbalimbali vya utalii na kwamba wamekuwa wakivitangaza kupitia matamasha mbalimbali ya utamaduni.
“Tumekuwa tukiandaa matamasha mbalimbali ya asili hapa Same, vikiwemo vyakula, mavazi na tamaduni nyingine za kabila la Wapare, kuonyesha jamii na Tanzania nzima kwamba ni vitu gani vinapatikana hapa Same,” amesema.