Ofisa Jeshi la Magereza akwaa kisiki kortini akitaka kurejeshwa kazini

Dodoma. Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma imeyatupa maombi ya askari wa Jeshi la Magereza aliyefutwa kazi mwaka 2022, Joel Runda Marivei ya kutaka Mahakama ifute uamuzi wa kumfuta kazi na mwajiri wake aamriwe kumrudisha kazini.

Katika maombi hayo, Marivei aliyekuwa na cheo cha Sajini (Senior NCO) alimshtaki Kamishna Mkuu wa Magereza (CGP) kama mjibu maombi wa kwanza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kama mjibu maombi wa pili.

Hata hivyo, katika uamuzi wake alioutoa Mei 17, 2024, Jaji Edwin Kakolaki aliyesikiliza maombi hayo aliyatupa baada ya kukubaliana na pingamizi moja la Kamishna Mkuu wa Magereza na AG kuwa maombi yana dosari kisheria.

Katika kiapo chao cha pamoja, wajibu maombi hao waliweka pingamizi wakieleza kuwa maombi hayajimudu na au yameletwa kabla ya wakati wake kwa vile mwombaji ameshindwa kutumia kwanza vyombo vya rufaa katika Jeshi Magereza.

Juni 6, 2016, Bundala aliajiriwa na Jeshi la Magereza na kufanikiwa kupanda vyeo hadi ngazi ya Sajini alipofukuzwa kazi jeshini Desemba 12, 2022.

Kwa mujibu wa barua ya kumfuta kazi, Jeshi la Magereza lilimtuhumu kwa makosa ya kinidhamu na kuwa amepoteza sifa za kuendelea kuwa askari wa kutegemewa, lakini katika mwenendo wa kesi, haikufafanuliwa kosa ni nini.

Hakuridishwa na uamuzi huo, ndipo akafungua maombi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma akisema hakupewa haki kamili ya kusikilizwa mbele ya kamati ya maadili, ambayo katika uamuzi wake ilifikia uamuzi wa kumfukuza kazi.

Katika kesi hiyo, aliwasilisha maombi matatu, moja Mahakama itoe amri ya kufuta uamuzi wa kumfuta kazi, mbili wajibu maombi walazimishwe kuzingatia sheria na wamrudishe kazini na tatu wazuiwe kuingilia ajira yake kwa namna yoyote.

Baada ya wajibu maombi kukabidhiwa nakala ya sababu za maombi hayo, waliwasilisha kiapo cha wakipinga uhalali wa kisheria wa maombi hayo na kuwasilisha pingamizi la awali.

Katika kiapo chao cha pamoja, wajibu maombi hao waliweka pingamizi wakieleza kuwa maombi hayajimudu na au yameletwa kabla ya wakati wake kwa vile mwombaji ameshindwa kutumia kwanza vyombo vya rufaa katika Jeshi Magereza.

Wakati wa mleta maombi alijiwakilisha mwenyewe bila wakili, wajibu maombi wote wawili walitetewa na Wakili wa Serikali, Kumbukeni Kiondo kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.

Akijenga hoja ya pingamizi hilo, Wakili Kiondo alisema sheria iko wazi kuwa pale ambapo vipo vyombo vya ziada vya kushughulikia mgogoro, mleta maombi alipaswa kupitia kwanza kwenye vyombo hivyo hadi vifikie mwisho.

Wakili huyo alisema kifungu cha 5(f) cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma za Magereza ya 1990, kuna Tume yenye mamlaka ya kusikiliza rufaa zinazoanzia kwenye chombo cha nidhamu.

“Mleta maombi (Marivei) alipaswa akate rufaa kwenye chombi hicho kwanza kupinga uamuzi huo wa CGP badala ya kuja Mahakamani kuomba marejeo ya uamuzi huo wa CGP,” alisema na kunukuu uamuzi wa kesi nyingine kama hiyo.

Mbali na hilo, lakini wakili huyo alisema kupitia barua ya Januari 12, 2023 kwenda kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Utumishi na Utawala Bora, kulikuwa na rufaa aliyoiwasilisha kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani haijatolewa uamuzi.

“Kitendo cha kuleta maombi mahakamani wakati rufaa yake bado inasubiri kutolewa uamuzi na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, muombaji alikuwa anaendesha farasi wawili kwa wakati mmoja jambo ambalo halikubaliki,” alisema.

Akijibu hoja hizo, Marivei alipinga hoja hizo akisema sio kweli kwamba alipaswa kukata rufaa kwa Kamishna, kwa cheo chake cha NCO, chombo cha mwisho cha rufaa kwa maofisa wa cheo hicho ni kwa CGP.

Katika hoja zake, aliendelea kueleza kuwa alipewa kibali na mahakama hiyo hiyo (Mahakama Kuu) Agosti 1, 2023 ya kufungua maombi hayo na haoni sababu mahakama hiyo ichukulie kama ni suala la rufaa wakati inayo mamlaka kuisikiliza.

Askari huyo kabla ya kufutwa kazi, aliendelea kueleza kuwa mahakama imepewa mamlaka hayo kupitia Ibara ya 30(3) ya Katiba ya Tanzania na mahakama inapaswa kujikita kwenye uhalali wa kisheria.

Hii kwa mujibu wa Marivei, ni pale ambapo mamlaka iliyotoa uamuzi (kama huo wa kumfuta kazi) ilizidisha mamlaka iliyonayo, kufanya makosa au kukiuka haki za msingi au ilifikia uamuzi usio wa haki ambao mtu mwenye busara asingeufikia.

Katika uamuzi wake, Jaji Kakolaki alisema amepitia kwa shauku mabishano ya pande hizo mbili na kurejea sheria mbalimbali ili kujibu hoja ya kama maombi hayo hayako sawa awa au yameletwa kabla ya muda wake mahakamani.

Jaji alisema kupitia mabishano hayo na viapo vilivyowasilishwa mahakamani, hakuna ubishi kuwa mleta maombi aliondolewa kazini na CGP Desemba 12, 2022 na wakati anaondolewa alikuwa akishikiliwa cheo cha Sajini au NCO.

Cheo hicho kwa mujibu wa Jaji, ni cha chini ya Mkaguzi Msaidizi wa Magereza ambaye mamlaka yake ya nidhamu ni sawa na CGP kama ilivyoelezwa katika kifungu cha 7(5) cha Sheria ya Polisi na Magereza na Kanuni zake.

Jaji alisema pia ni jambo lisilo na mashaka kuwa baada ya kutorishwa na uamuzi wa CGP wa kumfuta kazi, mleta maombi alikata rufaa kwa Katibu Mkuu wizara ya Utumishi na Utawala Bora kupitia barua aliyoiandika Januari 12, 2023.

Barua hiyo kwa mujibu wa Jaji, ndio iliyodokeza ukweli kuwa kabla ya kutuma rufaa yake kwa Katibu mkuu Utumishi na Utawala Bora, pia alikata rufaa kwa Katibu mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi bila kupatiwa majibu.

Jaji alisema pande zote mbili wote wanakubali kuwa chini ya kifungu 5(f) cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma ya Magereza kikisomwa pamoja na kifungu cha 9(2), kuna Tume yenye mamkala ya kusikiliza rufaa kutoka kamati za nidhamu.

Hata hivyo, Jaji alisema jambo ambalo limefanya pande hizo mbili zijikute pembe zao zimeng’ang’aniana ni kama kwa mazingira yaliyopo, Bundala alitakiwa kukata rufaa kwenye tume kwanza kabla ya kwenda mahakamani kuomba marejeo.

Jaji alisema Mahakama imeridhika kuwa, kwamba uamuzi wa CGP ambao mleta maombi anaupinga kupitia maombi ya marejeo, unaweza kukatiwa rufaa kwenye Tume inayotajwa kwenye sheria ambayo ni Tume Huru kusikiliza rufaa kutoka kamati za nidhamu.

Kulingana na Jaji na kama wasilisho la Wakili Kondo lilivyokuwa, ni msimamo wa sheria kuwa pale sheria inatoa nafasi ya uwepo wa vyombo vingine vya haki vya kupitia kutafuta suluhu, ni lazima pande mbili ziwe zimefika mwisho huko kwanza.

“Katika Mahakama hii haijalishi kama muombaji alikata rufaa kwa Katibu Mkuu Wizara ya Utumishi na Utawala Bora na Wizara ya Mambo ya Ndani, lakini sheria inatoa fursa ya kukata kwanza rufaa kwenye Tume huru,” alisema Jaji.

Jaji alisema mapitio ya uamuzi huo wa CGP yangeweza tu kurejewa na mahakama, kama mwombaji angekuwa amemaliza ngazi za rufaa zilizotakwa na sheria, hivyo kwa msimamo huo anakubaliana na pingamizi la wajibu maombi na kuyatupa maombi hayo.

Related Posts