Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud amesema umefika wakati Wazanzibari kujiamulia na kupanga mipango yao wenyewe ili watu wake waishi kwa uhuru.
Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alitoa kauli hiyo leo Jumapili, Mei 19, 2024 wakati akizungumza na viongozi wa chama hicho katika mikoa mitatu ya kichama ya Mjini Magharibi, Unguja.
Kwa mujibu wa Othman yapo mambo yanayofanywa ndani ya Muungano kwa hisani lakini yapo kinyume na Katiba, hivyo iwapo wakija viongozi ambao wataamua kufuata Katiba, Zanzibar haiwezi kuwa na chake.
Ametoa mfano wa masuala ya forodha, mafuta na gesi na bandari kwamba kwa mujibu wa Katiba vitu hivyo ni vya Muungano, lakini kwa sasa vinasimamiwa na Zanzibar pekee yake kutokana na hisani.
“Hutupaswi kwenda hivi kwa hisani, kwa hiyo tunapaswa kupigania kupata nchi yetu yenye mamlaka kamili ili Zanzibar iache kuishi kama hisani kwa vitu ambavyo ni muhimu kwa wananchi wake,” amesema Othuman, aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar.
Amesema wananchi wanaishi katika uduni kutokana na ukosefu wa maono ya viongozi, hivyo umefika wakati wajipange kupigania haki za Zanzibar, nazo watazipata kwa kuondoa chama tawala madarakani na kuweka viongozi wanaotokana na chama hicho, ambao wana dhamira ya kweli kuleta mabadiliko.
Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Ismail Jussa amesema kazi iliyopo mbele yao ni kuhakikisha wanajipanga kimkakati kuingia madarakani mwaka 2025 ili yanayoendelea Zanzibar yawe mwisho.
Hawawezi kufikia mamlaka kamili kama hawakushinda uchaguzi na hawawezi kushinda uchaguzi kama hawana takwimu kamili za wanachama wao, hivyo kuwataka viongozi wa ngazi ya majimbo kutumia miezi miwili kuanzia sasa kutambua wanachama wao kupitia nyumba kwa nyumba.
Miongoni mwa vitu wanavyotakiwa kubaini kwa wananchi hao ni pamoja na kuwa na kitambulisho cha Mzanzibari na kitambulisho cha mpiga kura ili kuweka mikakati ya ushindi.
“Sisi hatuendi kugonga mlango wa mtu, ila tutafanya namna na mbinu zetu, kikubwa tufanye kazi hiyo kwa weledi na kutambua wanachma wetu,” amesema Jussa.
Amesema kwa sasa umefika wakati kwamba yale yaliyokuwa yakifanywa akitaja dhuluma na udanganyifu vinafika mwisho baada ya uchaguzi wa mwaka 2025.
Jussa amesema kipindi kilichopita walikwa na kazi ya ujenzi wa chama kwa sasa wanafanya kazi ya kuimarisha chama na kinachofuata ni ushindi kuingia madarakani mwakani.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu mstaafu wa chama hicho Zanzibar, Ahmed Mazrui amesema lengo lao ni kuona wakiwa na Serikali inayotambua haki za Zanzibar lakini haitafikia huko bila kuwa na mamlaka kamili.
Mazrui ambaye pia ni Waziri wa Afya, amesema hata wajenge barabara za dhahabu Wazanzibari hawawezi kuridhika kama hawajapata haki ya nchi yao.
“Hata ufanyike ushawishi gani, sisi tunapigania haki ya Mzanzibari, nayo ni mamlaka kamili ya Zanzibar, hatukengeuki wala hatubadiliki na tukitimiza hayo tutakuwa tumesuuza roho ya Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad huko alipo,” amesema Mazrui
Amesema waliorithi majukumu hayo wana wajibu mkubwa kuendeleza aliyotamani kuyafanikisha Maalim kwani mpaka sasa kuna walemavu na mayatima, kisa wazee wao walikuwa wakipigania mamlaka kamili na atakayekwenda kinyume na hayo ataingia kwenye dhulma.
Naye Mwanasheria Mkuu wa chama hicho ambaye pia ni Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Omar Said Shaaban amesema wana kazi kubwa kuhakikisha chama hicho kinaongoza dola ya Zanzibar
“Hili halina mjadala wala halina mbadala na hii ndio kazi kubwa tunatakiwa kufanya mwaka 2025 na kuiondoa CCM.