Arusha. Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ameshauri uwepo utaratibu kwa watendaji wakuu wa taasisi za fedha watakaofanya vema kuachwa muda mrefu kwenye nafasi zao.
Amesema kufanya hivyo, kutaimarisha ufanisi wa taasisi hizo za fedha na kuwa na masilahi kwa wananchi, kupitia huduma mbalimbali.
Pendekezo hilo la Sumaye, linakuja ilhali kanuni za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zinataka mkurugenzi mtendaji wa benki nchini atumikie kwa kipindi kisichozidi miaka 10.
Sumaye ameyasema hayo wakati akitoa maoni katika mkutano mkuu wa 29 wa wanahisa wa Benki ya CRDB jana Jumamosi, Mei 18, 2024 jijini Arusha, baada ya kuwasilishwa kwa Taarifa ya ripoti ya wakurugenzi na taarifa ya hesabu zilizokaguliwa na gawio kwa mwaka 2023.
Katika kauli yake hiyo, Sumaye alimtaja Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela akisema ameonyesha uwezo mkubwa wa utendaji.
Kutokana na hilo, Sumaye aliyewahi kuwa mjumbe wa bodi ya benki hiyo, alipendekeza kufanyika kwa mabadiliko ya kanuni ili kutoa fursa kwa viongozi hao wakuu wa benki watakaofanya vizuri watumikie zaidi ya miaka 10.
Sumaye amejenga hoja hiyo kutokana na taarifa iliyotolewa kuonyesha mizania ya benki hiyo na kampuni zake tanzu imeimarika kufikia Sh13.3 trilioni mwaka 2023, ikiwa ni ukuaji wa asilimia 121, tangu Nsekela alipokuwa mkurugenzi.
Kadhalika, taarifa hiyo imeonyesha ukuaji katika viashiria mbalimbali vya kiutendaji, ikiwemo faida baada ya kodi ambayo imeongezeka kwa asilimia 560 na kufikia Sh422.8 bilioni mwaka jana.
Jambo hilo, kwa mujibu wa taarifa hiyo limesababisha kuongezeka gawio kwa hisa kutoka Sh5 mwaka 2018 hadi Sh50 mwaka 2023, sawa na ukuaji wa asilimia 900.
“Mzee (Dk Charles) Kimei (aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB) aliitoa mbali sana benki hii na kuifikisha pale alipoipokea Abdulmajid,” alisema Sumaye.
“Niliwahi kumwambia jambo hili Profesa (Florens) Luoga (Gavana mstaafu wa BoT ambaye alikuwa miongoni mwa wageni waalikwa katika mkutano huo), benki ni taasisi nyeti, tatizo dogo tu linaweza kuwa na athari kubwa mno,” alisema Sumaye.
Alisisitiza kama kiongozi mkuu wa benki kubwa ana maono na dira, ni vema aachwe aendelee kutekeleza.
“Najua kuna kitu BoT, cha miaka 10. Ninafikiri pawapo ruhusa kwa baadhi ya benki, viongozi wake wapewe muda zaidi kutekeleza maono yao,” alisema.
Hata hivyo, akizungumzia na Mwananchi leo Jumapili juu ya pendekezo hilo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba alisema muda wa ukomo kwa viongozi wa benki una manufaa makubwa kuliko kinyume chake.
“Ni kama ilivyo kwa uongozi wa juu wa nchi kama urais, muda wa ukomo unatoa nafasi kwa watu wengine kuongoza na kuleta mawazo mapya katika maendeleo ya taasisi husika,” amesema.
Amesema kwa bahati nzuri Tanzania ina watu wengi wenye elimu na uwezo wa kuleta matokeo makubwa, kama waliopo sasa, hivyo hamna wasiwasi juu ya uendelevu wa taasisi hizo.
“Wanaoonekana sasa katika benki zinazofanya vizuri ni matokeo ya kaunzishwa kwa kanuni hizo, pengine bila hivyo na wao wasingepatikana.
Utaratibu huu ni mzuri, unatengeneza mazingira ya watu kutengeneza warithi kwa kujua kuwa muda wao wa uongozi utakoma wakati fulani,” amesema.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Nsekela amesema mkakati mpya wa biashara umekuwa muhimu kwa mafanikio ya benki, ukifanya kazi kama ramani ya kuboresha utendaji kazi.
Nsekela pia amesema CRDB imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kukuza ujumuishi wa kifedha, kwa wajasiriamali na wafanyabiashara.
“Kupitia mpango wa IMBEJU, taasisi ya CRDB Bank Foundation imeboresha uwezeshaji kwa vijana na wanawake. Zaidi ya hayo, benki imeunda ushirikiano wa kimkakati ili kufadhili vyema miradi ya maendeleo nchini,” amesema.
Amesema malengo ya benki hiyo na kampuni zake ni kuongeza mchango wa kampuni tanzu zilizoanzishwa, kuboresha huduma kwa wateja na kuwekeza zaidi katika ubunifu wa kidijiti.