Dodoma. Kufuatia kauli ya ndugu wa marehemu Askofu Mkuu wa Makanisa ya Methodist Tanzania (TMC), Joseph Bundala kudai wana wasiwasi ndugu yao hakujinyonga na kutaka uchunguzi zaidi ufanyike, Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limesema bado linaendela na uchunguzi wa tukio hilo.
Askofu Bundala alikutwa amekufa akidaiwa jinyonga kwa kutumia waya wa simu Mei 16, 2024 ndani ya choo cha ofisi yake, iliyopo kwenye kanisa la Methodist, Mtaa wa Ipagala A jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Alchelaus Mutalemwa, Polisi walikuta nyaraka zilizoonyesha marehemu alijiua kutokana na madeni aliyokuwa nayo pamoja na mgogoro wa shule binafsi aliyoiuza.
Hata hivyo, jana Jumamosi, msemaji wa familia ya askofu huyo, Tito Kasuga alisema wana mashaka na kifo cha ndugu yao, kwani madeni hayawezi kusababisha ajiue kwa kuwa hakuna mtu ambaye hana madeni na hata Serikali inadaiwa.
Kauli hiyo iliungwa mkono na dada wa marehemu, Veronika Alexander ambaye alisema askofu huyo alimpigia simu na kumjulisha kuwa kuna mtu anamtishia maisha na akili yake imefika mwisho na muda mfupi kidogo wakapokea taarifa za kifo cha kaka yake.
Veronika aliitaka Serikali kufanya uchunguzi wa kifo hicho kwa kuwa ushahidi upo kwenye simu ya marehemu.
Leo Jumapili, Mei 19, 2024, alipoulizwa kuhusu wasiwasi huo wa ndugu, Kamanda Mutalemwa amesema bado wanaendelea na uchunguzi wa kifo hicho japo mpaka sasa hakuna mtu yeyote wanayemshikilia kuhusu tukio hilo.
Amesema kwa mujibu wa nyaraka walizozikuta kwenye ofisi ya askofu huyo, marehemu aliamua kujiua baada ya kuwa na madeni mengi ambayo alikuwa ameyaorodhesha.
“Bado tunaendelea na uchunguzi na mpaka sasa hakuna tunayemshikilia kuhusu tukio hilo, tukikamilisha uchunguzi wetu tutawajulisha,” amesema Kaimu Kamanda Mutalemwa.
Japo leo ni siku ya ibada, lakini hakuna ibada iliyofanyika kwenye Kanisa la Methodist Ipagala kufuatia msiba wa kiongozi wa kanisa hilo.
Mwananchi Digital limefika kanisani hapo saa 4 asubuhi na kukuta milango ya kanisa imefungwa kwa makufuli huku pakiwa kimya bila dalili za uwepo wa ibada.
Baadhi ya majirani na kanisa hilo wamesema si kawaida kanisa hilo kuwa kimya siku za ibada ila hali hiyo imetokana na msiba wa askofu huyo.
Kelvin Chenga, mmoja wa majirano hao amesema siku za nyuma kanisani hilo lingekuwa limejaa waumini kuanzia saa moja asubuhi hadi saa saba mchana kwa ajili ya ibada lakini leo hali ni tofauti kutokana na msiba.
Hata hivyo, Mwananchi imedokewa kuwa waumini wa kanisa hilo wamekwenda msibani Ihumwa ambako na inasemekana ibada inafanyika huko.
Mmoja wa wapangaji kwenye vyumba vilivyoko kwenye eneo la kanisa hilo ambaye ni mwanafunzi wa sekondari, Luka Chisebe amesema Askofu Bundala alikuwa ni kama baba yake na msiba huo umemuathiri na Jumatatu anatakiwa kufanya mitihani lakini hatoweza kwa kuwa anatakiwa kwenda kumzika askofu huyo.
Endelea kufuatilia Mwananchi Digital kwa habari na taarifa mbalimbali.