Ashikiliwa na polisi akidaiwa kuwachoma moto ndugu zake

Morogoro. Jeshi la Polisi mkoa wa Morogoro linamshikilia Paschal Elias (18) kwa tuhuma za kutaka kuwauwa ndugu zake watatu baada ya kuwamwagia kimiminika kinachodhaniwa kuwa cha mlipuko na kuwasababishia majeraha makubwa ikiwemo yeye mwenyewe.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Mei 20, 2024, Kamanda wa jeshi hilo mkoani Morogoro, Alex Mkama amesema tukio hilo lilitokea Mei 16, 2024 katika kijiji cha Gonja kilichopo kata ya Pemba, wilayani Mvomero.

“Kabla ya tukio hilo, aliwakusanya ndugu zake watatu kwa lengo la kuwapasha habari, badala yake aliwamininia kimiminika kinachodhaniwa kuwa ni mafuta yenye asili ya mlipuko na kusababisha kuungua kwa nyumba yao ya nyasi na kusababisha majeraha makubwa kwake na ndugu zake hao,” amesema.

“Majeruhi hao wamelazwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro na walitambulika kwa majina ya Mathias Elias (34), Agustino Elias (24), Anjela Elias (12) ambapo inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alikua na matatizo ya akili.

“Kwa mujibu wa ndugu wa mtuhumiwa aliyejitambulisha kwa jina la Paul Elias amesema taarifa za tukio hilo alizipata kupitia kwa jirani yake,” amesema kamanda huyo.

Amesema wakati ajali inatokea hakuwa mazingira ya nyumbani, lakini baadhi ya majirani walimpigia simu kuwa nyumbani kuna ajali ya moto, alipofika alikuwa moto umeunguza nyumba na ndugu zake wameokolewa wakiwa wameungua.

Amesema ndugu zake walikimbizwa hospitali ya wilaya Mvomero ambako walianza kutibiwa kabla ya kupewa rufaa kwenda hospitali ya rufaa ya mkoa.

Mwananchi limefika hadi hospitali ya rufaa ya mkoa na kuzungumza na majeruhi hao ambapo Agustino Elias amesema aliyewachoma ni ndugu yao wa damu.

“Alituita akasema nina tatizo mje niwaambie, kuna kikao cha familia, tukaenda pale sisi tukaingia ndani ila yeye hakuingia badala yake yeye akatufungia kwa nje akakimbia kuelekea ndani kwake baada ya kuona, hivyo nikapita dirishani nikawafungulia wenzangu nikiwasihi tukamuangalie ndani kwake.

“Tulipofika tukamkuta kajifungia kwenye nyumba yake, tukamsihi afungue mlango maana alisema ana jambo la kutuambia, akakataa akadai tusimlazimishe, sisi tulikua mbele ya mlango wa nyumba yake tukausukuma ule mlango kumbe mwenzetu hatukujua ndani alikua na petroli, akajimwagia yale mafuta na mengine aliyaacha kwenye dumu akalipua ule moto, kwa kuwa tulikua pale moto ukatupata,” amesema kijana huyo.

Kwa upande wake, Devotha Mshumbuzi ambaye ni muuguzi wa zamu katika hospitali hiyo, amethibitisha kuwapokea majeruhi hao wakiwa wane.

“Nakiri kupokea wagonjwa wanne kutoka Gonja, kata ya Pemba, walifika majira ya saa 7 usiku, na kwa sasa wako wodini na hali zao zinaendelea ingawa kuna wagonjwa wawili hali zao sio nzuri na tumewapa rufaa kwenda hospitali ya taifa ya muhimbili ili wakatibiwe zaidi kutokana na majeraha makubwa waliyoyapata,” amesema.

Related Posts