BAADA ya maswali mengi juu ya ndoa ya beki wa klabu ya Richards Bay inayoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini, Mtanzania Abdi Banda, mwenyewe kajitokeza na kufafanua ilivyokuwa.
Staa huyu amethibitisha kuachana na mkewe wa kwanza, Zabibu Kiba ikiwa ni moja ya swali linaloulizwa na mashabiki wengi hususan mitandaoni, baada ya kuona picha za harusi yake mpya.
Banda ameeleza kwamba alichana na Zabibu tangu mwanzoni mwa mwaka jana ingawa hakusema sababu za kuvunjika kwa ndoa yao.
“Harusi yangu ilikuwa Jumamosi ya Mei, 18, 2024 kwenye msikiti wa Kichangani, Dar es salaam. Mke wangu anaitwa Bi Maryam ni Mtanzania mwenye asili ya Tanga. (Ndoa) haikuhudhuriwa na mastaa kwa sababu walikuwa na majukumu yao ya kikazi ila walinisapoti sana,” amesema mchezaji huyo.
“Kuhusu binti yangu niliyezaa na mke wangu wa zamani Zabibu, anaishi na mama yake, kwani bado mdogo nikisema nimchukue atakuwa mnyonge, kwani kazi zangu haziniruhusu kukaa muda mwingi nyumbani.”
Alipoulizwa kuachana na Zabibu itakuwa mwisho wako wa kushabikia muziki wa Ali Kiba? Banda amejibu, “nilikuwa shabiki wa Ali Kiba kabla sijamuoa dada yake, hivyo nitaendelea kushabikia kazi zake, kwani anaimba muziki mzuri.”
Pia amejibu tetesi za chanzo cha kuachana na Zabibu zilizokuwa zinasemwa kwamba ilitokana na umbali, lakini Banda amesema: “Hiyo siyo sababu, niliishi nao muda mwingi, kikubwa hapo kila mtu ana amani, hivyo siwezi kuweka kila kitu mitandaoni.”
VIPI KUHUSU LIGI YA SAUZI
Banda amesema anafurahi kuona timu yake imesalia Ligi Kuu Afrika Kusini inayoisha wiki ijayo, kwani ilikuwa na ushindani mkali uliomfanya apambane zaidi kutimiza malengo yao.
“Ligi ya Afrika Kusini ni ngumu. Ukiona unapata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza, unakuwa unajitambua kipi unatakiwa kukifanya, tofauti na Tanzania ambako muda mwingi wachezaji wanakaa kambini,” amesema.
“Afrika Kusini kila mchezaji anajisimamia mwenyewe, kama unakuwa hujitunzi utapimwa kwa kiwango ambacho unakionyesha uwanjani, hivyo kila mchezaji anakuwa anatamani kuona timu inapata ushindi.
Banda anasema amejifunza mengi maisha ya wanasoka Afrika kusini, tangu alipojiunga kwa mara ya kwanza na Baroka 2017/18 akitokea Simba, kisha akarejea nchini kuja kujipanga upya 2021/22 ambapo akasajiliwa Mtibwa Sugar.
“Katika maisha kamwe usiruhusu kukata tamaa, kuna kipindi nilipitia majeraha, yaliyokuwa yameniweka nje takribani miezi sita, nikarudi nyumbani kujipanga upya, nikachagua Mtibwa ambayo niliona nitacheza kwa muda mwingi, malengo yangu yakafanikiwa kisha nikarejea tena Afrika Kusini katika klabu ya Chippa United.
“Kila nikiiangalia Mtibwa Sugar nafasi iliopo roho inaniuma msimu wa 2021/22, nilipoichezea niliishi vizuri na nilipata ushirikiano mkubwa” anasema Banda mchezaji wa timu ya Taifa Stars.
Vipi kuhusu anavyoiona Ligi Kuu? Anajibu “Kwa ujumla ipo vizuri ndio maana wachezaji kutoka mataifa mbalimbali, wanaichezea, ushindani ni mkubwa na inatazamwa kila kona, kwa sababu inaonyeshwa.
Coastal Union (2012–2014), Simba (2014-2017),Baroka (2017-2019), Highlands Park (2019/20),TS Galaxy (2020),Mtibwa Sugar( 2021-2022), Chippa United (2022/23),Richards Bay (2023/24).