BAADA ya kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho, Kocha wa Azam, Youssouph Dabo amesema kazi bado haijaisha kwani msimu huu wanalitaka kombe la michuano hiyo.
Azam FC ilifuzu hatua hiyo kwa ushindi wa 3-0 dhidi ya Coastal Union na sasa watakutana na Yanga iliyofanya hivyo kwa ushindi wa bao 1-0 mbele ya Ihefu.
Fainali hiyo kwa timu hizo inakuwa ya pili mfululizo baada ya msimu uliopita kukutana tena huko Mkwakwani jijini Tanga na Yanga kushinda bao 1-0 na kutwaa taji hilo.
Dabo amesema pamoja na kumaliza lengo la kwanza kutinga fainali, bado kazi ni ngumu katika kufikia malengo yao ya kutwaa ubingwa dhidi ya wapinzani wao.
Amesema kwa sasa benchi la ufundi linaendelea na program kuwaandaa wachezaji kiakili, kisaikolojia na kiufundi kuhakikisha mechi ya fainali hawafanyi makosa.
“Hatuwezi kuweka wazi mikakati yetu kwa sababu tuna mpinzani mwingine mbele, tunaenda kujipanga na kuona jinsi ya kushinda taji hili muhimu kwetu,” amesema na kuongeza:
“Coastal Union wametupa upinzani mkali ukizingatia beki yao ni ngumu kupita, lakini mbinu zetu ziliweza kutupa matokeo mazuri na sasa tunaitaka fainali.”.
Kuhusu kutoa nafasi kwa wachezaji, Kocha huyo raia wa Senegal, amesema ni uamuzi wa benchi la ufundi kupanga mchezaji gani aanze au kusbiri kulingana na mchezo husika.
“Kila mchezaji yuko hapa kutimiza majukumu na wanapaswa kufanya hivyo kwa wajibu wao kwahiyo leo unaweza kupata dakika 30 kesho tano lakini kila mmoja anayo nafasi yake,” amesema Msenegar huyo.