Muda mfupi baada ya Kiongozi wa juu wa kisiasa na kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei kumtangaza kuwa kaimu Rais, Mohammad Mokhber ameongoza kikao chake cha kwanza cha baraza la mawaziri. Katika kikao hicho Mokhber amewahakikishia raia wa taifa hilo kuwa hakuna kitakachoharibika baada ya kifo cha Ebrahim Raisi.
Soma zaidi: Risala za rambirambi zatolewa kutoka kote duniani kutokana na kifo cha Rais wa Iran Ebrahim Raisi
Mohammad Mokhber amesema, “Hili ni tukio zito la kusikitisha kwetu sote. Linasababisha huzuni na uchungu lakini kuhusu suala la utawala na mwenendo wa nchi, watu wote wanapaswa kuwa na uhakika kuwa hakutakuwa na tatizo lolote.”
Kiongozi huyo wa muda wa Iran amesema nchi hiyo itaendelea kusonga mbele chini ya uongozi wake na kuwa kila mmoja anapaswa kuendelea na majukumu yake licha ya msiba huo. Ameongeza kuwa kwa namna yoyote ile, kilichotokea hakipaswi kuingiliana na serikali na uendeshaji wa taifa la Iran.
Soma zaidi:Helikopta iliyombeba rais wa Iran yapata ajali, haijulikani ilipo
Mokhber, sasa anashikilia wadhifa huo wa kaimu Rais kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kuitishwa ndani ya siku 50.
Kulingana na ripoti ya shirika la habari la Iran la Tasnim, ibada ya kuwakumbuka Rais Ebrahim Raisi na Waziri wa Mambo ya Kigeni Hossein Amirabdollahian zinapangwa kufanyika Jumanne kaskazini magharibi mwa mji wa Tabris na kwenye mji wa Qom.
Siku ya maziko ya viongozi hao waliokufa Jumapili kwa ajali ya helikopta bado haijawekwa wazi wakati raia nchini humo wakikusanyika katika mji mkuu Tehran kuomboleza kifo cha rais wao.
Mataifa ya Ghuba yatoa pole kwa Iran
Katika hatua nyingine, mataifa ya Ghuba jirani na Iran, yametoa salamu za rambirambi yakiomboleza kifo cha Raisi na waziri wake wa mambo ya nje.
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa nalo limekaa kimya kwa dakika moja kama alama ya kutoa heshima kwa kiongozi wa Iran aliyekufa.
Saudi Arabia iliyorekebisha uhusiano wake na Tehran mwaka uliopita baada ya mpasuko wa muda mrefu, imetoa pole kwa kaimu rais wa Jamhuri ya watu wa Iran Mohammad Mokhber kufuatia msiba huo.
Naye Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Mohammed bin Zayed Al Nahyan amesema mataifa ya Falme za Kiarabu yanaungana na watu wa Iran katika wakati huu mgumu.
Kwa upande wake kiongozi wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani, kupitia jukwaa la mtandao wa kijamii wa X, amezitaja habari hizo za msiba kuwa za kuumiza.
Salamu nyingine za rambirambi zimetoka kwa mfalme wa Bahrain, Hamad bin Isa Al Khalifa, Oman na kutoka kwa katibu mkuu wa baraza la ushirikiano wa nchi za Ghuba Jassem al-Budaiwi.