Huduma hisa, hati fungani kupatikana matawi ya NMB

Dar es Salaam. Ili kuongeza ushiriki wa wananchi katika soko la mitaji nchini, Benki ya NMB imesaini makubaliano na kampuni ya uwakala na ushauri wa uwekezaji ya ORBIT Securities, ili kuiwakilisha katika soko la hisa la Dar es Salaam (DSE).

Hatua hiyo inakuja baada ya NMB kupata idhini kuwa wakala wa madalali wa soko la hisa la Dar es Salaam kutoka Benki kuu ya Tanzania (BoT) pamoja na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA).

Hivyo, hisa na hati fungani zitauzwa kupitia matawi yote ya NMB, kwa niaba ya Madalali wa Soko la Hisa ambapo itapokea oda za uuzaji au ununuaji wa hisa na hati fungani, kwa niaba ya madalali hao.

Akizungumza leo kwenye hafla fupi ya utiaji saini makubaliano hayo iliyofanyika makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna amesema kwa idhini hiyo itawafanya kuuza na kununua hisa na hati fungani katika matawi yake yote yaliyopo nchini.

“Hivyo Mtanzania yeyote atapata huduma za kuuza na kununua hisa na hati fungani za kampuni mbalimbali zilizopo kwenye soko la mitaji kwenye matawi 231,” amesema.

Zaipuna amesema  Watanzania asilimia pekee ndio wanaotumia soko la mitaji kuwekeza. Hivyo, amesema hatua hiyo itawafikia Watanzania wengi zaidi.

“Hii ni hatua kubwa ya kuwaingiza Watanzania wengi zaidi kwenye pamoja na wawekezaji kwenye soko la mitaji hapa nchini,” amebainisha.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Orbit Securities, Godfrey Gabriel amesema hatua hiyo inaenda kuleta urahisi wa soko la mitaji kwa Watanzania.

Amesema watu waliopo nje ya Dar sasa wataweza kupata huduma hiyo jambo ambalo litamaliza ile changamoto ya hapo awali iliyowalazimu kufika jijini Dar es Salaam kwanza ili kupata huduma hiyo.

“Ushirikiano huu unafungua milango kwa watu binafsi na wafanyabiashara ikiwa inaenda sambamba na mpango wa maendeleo ya sekta ya fedha ya Serikali kwa kuimarisha masoko haya na ujumuishaji wa fedha,” amesema.

Amesema lengo ikiwa kuwafikia Watanzania angalau asilimia tano waweze kupata bidhaa na huduma ya soko la mitaji hadi ifikapo mwaka 2030.

Aidha, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Mary Mniwasa amesema awali kulikuwa na kilio kutoka kwa wawekezaji kwamba soko la hisa limekuwa likihusisha watu wa Dar pekee lakini ukweli soko hilo ni la watanzania wote.

“Makubaliano haya yataongeza uwekezaji katika soko la hisa na ongezeko la ufanisi katika utoaji huduma ambapo wawekezaji wengi watafikiwa kwa urahisi zaidi,” amebainisha.

Naye, Mwakilishi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana CMSA, Alfred Mkombo amesema sekta ya fedha inaenda kupata mabadiliko kutokana na uanzishwaji wa huduma hiyo.

Amesema jambo hilo linazidi kuiweka Tanzania kwenye ramani ya soko la mitaji duniani:”Tunalenga kuongeza ushiriki wa wananchi katika soko la mitaji na pia wananufaika” amebainisha CPA Mkombo.

Related Posts