Iran yaomboleza kifo cha Ebrahim Raisi – DW – 20.05.2024

Kifo cha Raisi kimetangazwa na televisheni ya taifa ya Iran baada ya juhudi za kufika eneo la tukio lililochukua saa kadhaa kutokana na hali mbaya ya hewa.

Kiongozi huyo wa Iran, Waziri wake wa mambo ya nje Hossein Amirabdollahian, Gavana wa mkoa wa Azerbaijan mashariki uliopakana na Iran na maafisa wengine wamefariki katika ajali hiyo ya helikopta iliyotokea Jumapili.

Soma zaidi: Helikopta iliyombeba rais wa Iran yapata ajali, haijulikani ilipo

Msafara huo ulikuwa ukielekea katika mji wa Tabriz kaskazini magharibi mwa Iran, baada ya Raisi kushiriki katika hafla ya ufunguzi wa mradi wa pamoja wa bwawa la kuzalisha umeme kwenye eneo la mpakani na Arzebaijan.

Hofu ilitanda mchana kutwa baada ya helikopta hiyo ambayo kulingana na shirika la habari la Tasnim ilikuwa na jumla ya abiria tisa akiwemo kiongozi huyo kupoteza mawasiliano. Hata hivyo bado sababu za kutokea kwa ajali hiyo bado hazijatolewa.

Juhudi kubwa za kulifikia eneo la ajali zilicheleweshwa na hali mbaya ya hewa

Mapema Jumatatu, mamlaka za Uturuki zilchapisha video za droni zilizoonesha kile kilichoonekana kuwa moto na mabaki ya helikopta hiyo kilometa 20 kusini mwa mpaka wa Iran na Azerbaijan katika eneo lenye mlima mkali.

Rais wa Iran Ebrahim Raisi amefariki dunia katika ajali ya helikopta
Picha inayoonesha eneo ilikotokea ajali ya helikopta iliyosababisha kifo cha Rais wa Iran Ebrahim RaisiPicha: Iranian Red Crescent Society/Anadolu/picture alliance

Masalia ya chombo hicho yamepatikana baada ya juhudi za usiku kucha za kulifikia eneo hilo huku hali ya hewa ikiripotiwa kuwa mbaya. Mkuu wa hilali nyekundu wa Iran, Pir Hossein Kolivand, alinukuliwa akisema kwamba hakukuwa na dalili zozote za abiria wa helikopta hiyo kuwa hai baada ya timu za uokoaji kufika mahali ilikotokea ajali.

Soma zaidi: Rais wa Iran aripotiwa kufa katika ajali ya helikopta

Kutokana na msiba huo, Kiongozi mkuu wa kidini na kisiasa wa Iran Ali Khamnei  ametangaza siku tano za maombolezo ya kitaifa.

Ajali ya helikopta Iran
Juhudi za uokoaji za kufikia eneo la ajali ya helikopta aliyokuwamo Rais wa Iran, Ebrahim RaisiPicha: Stringer/WANA via REUTERS

Khamenei pia amemthibitisha makamu wa kwanza wa Rais Mohammad Mokhber kuwa kiongozi wa mpito wa taifa hilo hadi uchaguzi utakapofanyika huku ,mjumbe wa ngazi ya juu katika masuala ya Nyuklia ya Iran Ali Bagheri akiteuliwa kukaimu nafasi ya waziri wa mambo ya kigeni , sasa taifa hilo lina muda usiopungua siku 50 kufanya uchaguzi ili kumpata mrithi wa Raisi.

Related Posts