Kamati ya Bunge yaupongeza Mfuko wa WCF kutoa fidia kwa Wafanyakazi

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeutaka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) uliopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kuogeza jitihada ya kusajili wanachama wapya ili kuhakikisha nguvu kazi ya Taifa inalindwa na fidia inatolewa kwa wafanyakazi wanaopata ugonjwa au ajali inayotokana na kazi.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Fatuma Toufiq, wakati walipotembelea Makao Makuu ya Ofisi za WCF, jijini Dodoma kwa lengo la kupata uelewa wa masuala ya fidia kwa wafanyakazi.

Amesema kuwa, Sekta binafsi inakuwa kwa kasi na imeendelea kuleta tija katika kuchangia kodi na kutengeneza ajira zaidi, hivyo amesisitiza mfuko huo kuhakikisha unasajili waajiri wengi zaidi katika sekta hiyo.

Vile vile, ameipongeza WCF kwa kulipa fidia kwa wafanyakazi wanaostahili, pamoja na kuwa na utaratibu wa kutoa elimu kwa makundi mbalimbali kuhusu elimu ya fidia kwa wafanyakazi.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Riziki Lulida ametoa rai kwa waajiri kutambua wajibu wa kutoa michango kwa ajili ya wafanyakazi wao ili ikitokea madhila yatokanayo na kazi mfuko huo wa WCF uweze kutoa fidia.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Dkt. John Mduma ameahidi kufanyia kazi maoni ya kamati huku akieleza kuwa WCF imejipanga kusajili wanachama wengi zaidi kwa kuimarisha mifumo ya kutolea huduma ambayo itawawezesha Waajiri wengi zaidi kujisajili.

Related Posts