BEKI wa kushoto wa Yanga, Nickson Kibabage amesema kwamba alijikuta hospitali baada ya kupoteza fahamu katika mchezo wa Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Ihefu SC jana, lakini hakumbuki nini kilitokea kabla ya hapo.
Kibabage aliyeanguka mwishoni mwa kipindi cha kwanza cha mchezo huo, mwanzoni mwa msimu huu alikuwa akiichezea Singida Fountain Gate kabla ya kutua Yanga katika dirisha dogo anakocheza kwa mkopo.
Mchezaji huyo ambaye amefunga bao moja na asisti nne, amekuwa na uwezo mzuri kulinganisha na Joyce Lomalisa ambae wanacheza wote nafasi moja.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kibabage amesema anachokumbuka ni kwamba alijikuta yupo hospitali, lakini kabla ya hapo alianza kuhisi maumivu makali ya kichwa katikati ya mchezo.
Amesema kwamba hiyo ndiyo mara yake ya kwanza kutokewa na hali hiyo akiwa uwanjani tangu aanze safari ya soka.
“Nilizinduka nikiwa hospitali na daktari aliniambia ni hali ya kawaida nisiwe na hofu. Pia walinipatia dawa za kutuliza maumivu na kutundikiwa dripu za maji,” amesema.
“Nilitoka hospitali saa saba usiku nikiwa mzima kabisa. Kwa sasa niko salama sihisi maumivu yoyote yale na niko tayari kwa michezo ijayo kwani daktari hakuniambia chochote baada ya kuruhusiwa,” amesema Kibabage.
Mama Mzazi wa beki huyo, Flora Ngwido amesema wakati mechi hiyo inachezwa nyumbani hakukuwa na umeme, lakini alishangazwa na wingi wa simu.
“Nilishtuka sana kuona napigiwa na watu wengi kwa wakati mmoja, lakini baadaye na nilipojua tu mtoto wangu amepata tatizo niliamua kuizima, kwani nilijua hakuna nitakayempata kwa wakati huo,” amesema.
“Wanapomaliza mechi kwa kawaida anaanza kushika na simu baada ya saa moja, hivyo muda huo ulipopita tu nilikaongea na daktari na kuniambia kuwa hali yake iko shwari na nisihofu.”
Yanga inarejea Dar es Salaam leo ikitokea Arusha ikijiandaa kucheza dhidi ya Dodoma Jiji, Mei 22 saa 10:00 Jioni.